In Summary

•Mkewe Alikiba amefuta picha zote za msanii huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya laki mbili.

•Amina aliwasilisha kesi ya talaka katika mahakama ya Kadhi ya Mombasa mapema mwaka huu.

Amina Khalef na Alikiba
Image: HISANI

Bi Amina Khalef, mke wa staa wa Bongo Alikiba amewaacha wengi na maswali chungu nzima  baada ya kufuta picha zote za msanii huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya laki mbili.

Isitoshe, mzaliwa huyo wa eneo la Pwani ya Kenya pia amechapisha ujumbe wenye maana fiche kwenye Instastori zake.

"Huru rasmi!" aliandika siku ya Jumanne.

Ingawa Bi Amina hajatoa maelezo zaidi, ujumbe huo na matukio ya hivi punde kwenye ukurasa wake wa Instagram yamechukuliwa kama ishara ya kukamilika kwa talaka yake na baba ya watoto wake wawili.

Amina aliwasilisha kesi ya talaka katika mahakama ya Kadhi ya Mombasa mapema mwaka huu baada ya kuwa kwa ndoa na Alikiba kwa miaka mitatu.

Mama huyo wa watoto wawili alitaka kuvunja ndoa yake na Kiba akilalamikia msongo wa mawazo na kutelekezwa.

Wawili hao walifunga ndoa chini ya Sheria ya Kiislamu mnamo Aprili 19, 2018, katika harusi ya kifahari iliyofanyika Mombasa na baadaye wakaendelea kuishi kama wanandoa jijini Dar es Salam Tanzania.

Wanandoa hao walibariki na mtoto wa kiume mnamo Februari 19, 2019.

Katika ombi la talaka lililowasilishwa Januari 8, 2021, Amina alidai kuwa Kiba hakuwa akiwajibikia watoto wao ifaavyo. Aliongeza kuwa fedha za matumizi alizotuma mwimbaji huyo hazikutosha na zingekuja baada ya mvutano mkubwa kati yao.

Amina alidai Sh200,000 za matumizi ya kila mwezi kwa ajili ya malezi ya watoto wao wawili. Pia alimtaka Kiba alipie bima ya matibabu kwa watoto wao.

Pia aliomba ndoa yao ivunjwe na mahakama ya Kadhi.

Alisema Kiba hakushughulika na hakutoa fedha zozote za utunzaji wakati alikuwa amebeba ujauzito wa mtoto wao wa kwanza na kwa kiasi kikubwa hakushughulika na hali yake wala ya mtoto wao.

View Comments