In Summary

•Matubia amefunguka kuhusu talaka yake ghali na ya kuchosha na aliyekuwa mume wake, rubani Kennedy Njogu.

•Matubia alifichua kuwa talaka yake na baba huyo wa bintiye ilimgharimu takriban Sh300,000 na pia ulimuathiri sana kisaikolojia.

Jackie Matubia na aliyekuwa mumewe Kennedy Njogu
Image: HISANI

Muigizaji maarufu wa Kenya Jackie Matubia amefunguka kuhusu talaka yake ghali na ya kuchosha na aliyekuwa mume wake, rubani Kennedy Njogu.

Matubia na Njogu walikuwa wanandoa kwa takriban nusu muongo kabla ya kuachana rasmi mapema mwaka wa 2019 kwa sababu ambazo hazijafichuliwa.

Katika mahojiano na Nairobi News, muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High alifichua kuwa mchakato wa talaka yake na baba huyo wa bintiye wa kwanza ulimgharimu takriban Sh300,000 na pia ulimuathiri sana kisaikolojia.

“Nilitumia takriban Sh300,000 kwa mchakato huo, hiyo ingebadilika kulingana na kesi yako. Ikiwa nyinyi watu mna mali pamoja, kuna tatizo la usaidizi wa watoto… Kuna mengi tu. Kuna vikao vingi na kadhalika,” Matubia alisema.

Aliongeza, "Yangu ilikuwa ya kutia kiwewe kwa sababu ilikuwa wakati wa Covid-19, kwa hivyo kesi yako ikitajwa, huwezi kwenda kortini, unafanya mtandaoni, kisha inaahirishwa. Jeraha hilo lilinipata sana.”

Muigizaji huyo mahiri alibainisha kuwa mchakato wa talaka nchini Kenya ni ghali sana na una shughuli nyingi na kufuatia hilo akawashauri watu kufikiria kwa kina kabla ya kupiga hatua ya kufunga ndoa.

"Usiwe na haraka, na ikiwa unaweza, kuwa wazi juu yake. Nilikuwa wazi tangu siku ya kwanza hata kabla ya uchumba. Sikuwa na hakika kwamba ningeshuka kwenye barabara hiyo ya harusi ya kanisani. Ikiwa mtu amechumbiwa kwa miaka 10 na bado hajaoa, watu wanapaswa kuelewa kwamba baadhi ya watu wanaogopa… Ningekaa na mtu nyumbani kwa zaidi ya miaka 15 kabla sijaamua kufanya harusi,” alisema.

Bi Matubia na Njogu ambaye ni rubani walikuwa wameoana kwa miaka kadhaa hadi 2019 na wana binti mmoja pamoja, Zari Wanjiku.

Takriban miaka mitatu baada ya kuachana na rubani huyo, mwigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High alimtambulisha mwigizaji mwenzake Blessing Lungaho kama mpenzi wake mpya mnamo Februari mwaka jana na wawili hao walijaliwa kupata mtoto pamoja miezi michache baadaye.

Uhusiano wa Bi Matubia na Lung’aho hata hivyo haukudumu kwa muda mrefu kwani walitengana mapema mwaka huu huku mama huyo wa watoto wawili akiwa tayari anadaiwa kuwa kwenye mahusiano na mwanamume mwingine.

View Comments