In Summary

•Majambazi hao ambao walikuwa wamejihami kwa bunduki walivamia kanisa hilo wakati ibada ilikuwa ikiendelea.

• mhubiri alionekana mwenye mshangao na wasiwasi kabla ya kujiunga na waumini wengine kupiga magoti.

Picha ya Kanisa
Image: BIBLE STUDY TOOLS

Genge la majambazi sita walivamia kanisa moja la Seventh-Day jijini Johannesburg, Afrika Kusini siku ya Jumamosi.

Majambazi hao ambao walikuwa wamejihami kwa bunduki walivamia kanisa hilo wakati ibada ilikuwa ikiendelea.

Mhubiri alikuwa akitoa mahubiri yake wakati majambazi hao walipoingia, matukio yalinaswa kwenye kamera za CCTV.

"Kwa nini Yesu aende..." mhubiri huyo alisikika akisema kabla ya kunyamaza ghafla pindi baada ya kuwaona majambazi hao wakiingia.

Kisha majambazi hao wakaamuru washarika wote wapige magoti. Katika video iliyoenezwa mitandaoni, mhubiri alionekana mwenye mshangao na wasiwasi kabla ya kujiunga na waumini wengine kupiga magoti.

Inaaripotiwa kuwa majambazi hao waliiba simu na pochi za waumini hao. Pia waliiba sadaka na pesa za zaka.

Kanisa hilo lilitoa taarifa baada ya ibada na kuwataka waumini kuendelea kuwa na umoja wakati wakitegua tukio hilo.

"Kanisa lingependa kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kuwa hili nalo litapita. Hakuna kinacho dumu milele. Kama viongozi, tunaombea kanisa kuungana katika nyakati kama hizi, tukisaidiana kimaadili na kimatendo," taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa kanisa hilo ilisoma.

Baada ya wizi, inasemekana mhubiri aliendelea na ibada ya kanisa ingawa waumini walikuwa wamejawa na kiwewe.

View Comments