In Summary

•Akothee alionyesha sahani yenye chakula kizuri alichokuwa amemwandalia mwanamume huyo ambaye aliwahi kuchumbiana naye kwa muda.

•Akothee alikuwa ameonyesha moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook akimpikia Nelly Oaks Ijumaa jioni.

Akothee na meneja wake Nelly Oaks
Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amejigamba kuwa mwanamke anayeelewa vyema tumbo la meneja wake Nelly Oaks.

Siku ya Jumamosi, mama huyo wa watoto watano alionyesha sahani yenye chakula kizuri alichokuwa amemwandalia mwanamume huyo ambaye aliwahi kuchumbiana naye kwa muda.

Katika sahani hiyo, kulikuwa na wali, kuku, kabichi na saladi.

"Jamani, hivi ndivyo meza ya Nelly Oaks inavyoonekana. Mimi ndiye mwanamke pekee ninayejua kutunza tumbo lake,” Akothee alisema kwenye video hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika video hiyo, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 aliendelea zaidi kuthibitisha na mpenzi huyo wake wa zamani ikiwa alipenda chakula hicho na ikiwa alikuwa ame’miss kupikwa naye.

"Unakipenda? Unapenda? Ume’miss chakula changu, sivyo?,” alimuuliza Nelly Oaks.

Meneja huyo wake alijibu, "Bila shaka."

Akothee na Nelly Oaks wameonekana wakiwa na ukaribu sana katika wiki chache za hivi majuzi na hivyo kuzua shauku kubwa kutoka kwa mashabiki kuhusu uhusiano wao wa sasa. Mbali na Nelly kuwa meneja wa mwimbaji huyo, pia alichumbiana naye kwa muda hadi mapema mwaka jana walipothibitisha kuachana kwao.

Mama huyo wa watoto watano alikuwa ameonyesha moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook akimpikia Nelly Oaks Ijumaa jioni.

Wakati wa kipindi hicho alichorekodi kutoka jikoni mwake, mwanamuziki huyo alionekana akitayarisha milo kadhaa huku akicheza muziki wa Kijaluo.

Ingawa Nelly Oaks hakuwa jikoni pamoja naye, ni wazi kwamba alikuwa karibu tu kwani mwanamuziki huyo alisikika akiongea naye na kumuuliza anataka kula nini.

“Nampikia Nelly... Nelly, Nelly Oaks.. nakupikia chakula cha jioni nini?? Kifua cha kuku? , kuku mzima, una mlo gani usiku huu?,” Akothee alisikika akisema.

Meneja huyo wake alionekana kukubali kula kuku, wali na saladi kwa chakula cha jioni.

“Na ungetaka chakula chako cha jioni kiandaliwe saa ngapi? Saa sita, saa saba?,” Akothee alisikika akimuuliza Nelly Oaks.

Kisha aliendelea na kupika na kucheza densi huku akirekodi matukio yote. Mtoto mdogo pia alionekana akizungukazunguka kwenye video hiyo ya moja kwa moja.

Wakati wa kipindi hicho cha moja kwa moja, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alisikika akidai kuwa Nelly Oaks huwa mbaya akiwa na njaa.

“Samahani, nilikusahau kwa sababu Nelly wangu ana njaa, na akipata njaa anakuwa mtu mbaya sana,” Akothee alisikika mwanamuziki huyo akiwaomba radhi mashabiki wake baada ya muziki aliokuwa akiupiga kukatika.

View Comments