In Summary

•Akothee alishiriki video ya mfanyakazi wake akivuna malenge  ambayo alifichua kuwa ni mzungu huyo alipanda.

•Akothee alifichua kuwa alikusudia kuchukua picha ya malenge hayo na kumtumia mzungu huyo kutoka Uswizi.

Akothee na mkewe Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amedokeza kuwa bado ana mawasiliano na mumewe Denis Schweizer hata kukiwa na tetesi za kuachana kwao.

Siku ya Jumanne, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alishiriki video ya mfanyakazi wake akivuna malenge  ambayo alifichua kuwa ni mzungu huyo alipanda.

“Ona budho ya Omosh. Omosh to lwete ber,” Akothee aliandika kwa lugha ya Kijaluo kwenye video hiyo aliyoshiriki kwenye Instastories zake.

Kumaanisha, “Ona malenge ya Omosh. Mkono wa Omosh ni mzuri kwa kile anachofanya,.”

Katika video hiyo, mama huyo wa watoto watano alisikika akimueleza mfanyikazi aliyekuwa akivuna malenge hayo kuwa ni mumewe ndiye aliyeyapanda.

Aidha, aliendelea kufichua kuwa alikusudia kuchukua picha ya malenge hayo na kumtumia mzungu huyo kutoka Uswizi.

“Unajua hizo ni Omondi alipanda, tena alitoka nayo Uswisi. Acha nimpigie picha nimtumie. Kuna ngapi?” mwimbaji huyo alisikika akimwambia mwanaume huyo aliyekuwa ameshika malenge mawili makubwa.

Pia alishiriki video zaidi za yeye akijadiliana na mfanyakazi huyo wa shambani na kumpa maelekezo walipokuwa wakizunguka shambani.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Haya yanajiri huku kukiwa na tetesi nyingi za kuvunjika kwa ndoa ya mwanamuziki huyo na mumewe Denis 'Omosh' Schweizer. 

Wiki jana hata hivyo, Akothee alisikika akishangaa  ni kwa nini watu wanadai kuwa ameachana na  mzungu huyo  ilhali yeye mwenyewe bado hajasema.

“Na kwa nini wanadhani tumeachana? Ata sijasema tumeachana! Sijasema tumeachana na wameanza kuniambia ndio ‘Ojingo wa 8’,” alisikika Akothee akisema kwenye video ambayo alichapisha Instagram.

Uhusiano wa sasa wa wawili hao haujulikani wazi kwani bado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu hali ya ndoa yao. Hata hivyo, kumekuwa na tetesi nyingi kwamba ndoa hiyo haipo tena na kwamba hawako katika maelewano mazuri.

Vitendo vya hivi majuzi kwenye mitandao vimezidisha tetesi za kuachana huku wanamtandao wakiwa na shauku kubwa ya kupata majibu.

Baadhi ya mambo ambayo yamewaacha watu wakizungumza ni Akothee kukiri hajakuwa sawa kisaikolojia katika miezi michache iliyopita, mwimbaji huyo kuacha kujitambulisha kama  ‘Bi Omosh’ kwenye Instagram na akaunti ya Omosh kuzimwa.

Akaunti ya Instagram ya Mister Omosh ilizimwa siku ya Jumatatu na kuzidisha uvumi kwamba kunaweza kuwa na matatizo fulani ambayo bado hayajafichuliwa. Akaunti hiyo ilikuwa na takriban wafuasi 72,000 kabla ya kutoweka. Hata hivyo, haijulikani ikiwa akaunti imezimwa kwa muda au kabisa.

Akothee tayari alikuwa ameacha kufollow akaunti hiyo kabla haijazimwa na pia alikuwa amefuta picha kadhaa za mume huyo wake mzungu.Mama huyo wa watoto watano pia alikuwa amefanya mabadiliko kadhaa kwenye akaunti yake ya Instagram, akiondoa jina 'Mrs Omosh' kutoka kwa wasifu wake.

View Comments