In Summary

•"Nilienda dukani kwa ajili ya familia yangu Kajala, Paula na Zuuh Konde. Nawapenda nyie," Harmonize alisema.

•Bosi huyo wa Kondegang aliwanunulia Paula na mama yake Kajala nguo  zinazofanana za rangi nyeusi. 

Harmonize, Zuuh Konde na Paula Kajala
Image: INSTAGRAM

Upendo na furaha vinaonekana kuzidi kuongezeka kwenye nyumba ya staa wa bongo Harmonize kadri siku zinavyosonga.

Siku za hivi majuzi Harmonize ameonekana mwenye bashasha hasa baada ya mchumba wake Kajala Masanja kurudiana naye takriban miezi mitano iliyopita. Kajala alimkubali tena mwimbaji huyo baada ya kuomba msamaha.

Ili kuonyesha upendo wake mkubwa kwa familia yake, staa huyo ambaye kwa sasa yupo katika ziara ya kikazi nchini Uingereza alifika dukani jijini London na kununulia familia yake nguo mpya. Miongoni mwa aliowanunulia nguo ni pamoja na mkewe Kajala, bintiye wa kambo Paula na bintiye wa kuzaa Zuuh Konde.

"Nilienda dukani kwa ajili ya familia yangu Kajala, Paula na Zuuh Konde. Nawapenda nyie," Harmonize alisema kwenye Instagram

Aliambatanisha ujumbe huo na video kadhaa zinazoonyesha fungu la nguo ambazo alinunulia familia yake.

Paula ambaye bila shaka ni miongoni mwa watakaonufaika na ziara ya Harmonize ya Uingereza anaonekana tayari ameshaingia vyema kwenye familia ya msanii huyo na kukubali kuwa binti yake wa kambo. Hivi majuzi uhusiano kati ya wawili hao ambao awali walikuwa hawapatani umeonekana kuimarika.

"@realpaulakajala & @zuuh_konde DADAHOOD❤❤ Nawapenda wasichana wangu!!!👩👩" Harmonize aliandika chini ya video iliyoonyesha nguo mpya ambazo aliwanunulia mabinti zake Paula na Zuuh.

Bosi huyo wa Kondegang aliwanunulia Paula na mama yake Kajala nguo  zinazofanana za rangi nyeusi. 

"Ni mimi tu najua jinsi wanavyopendana!" alisema.

Paula ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 20 sio binti halisi wa Harmonize. Baba mzazi wa mwanamitindo huyo ni mtayarishaji wa muziki P-Funk Majani ambaye alichumbiana na Kajala takriban miongo miwili iliyopita.

Zuuh ambaye jina lake halisi ni Zulekha Nasra kwa upande mwingine ni binti wa kuzaa wa staa huyo wa Bongo. 

Sio mengi yanayojulikana kumhusu mamake Zuuh, Official Shanteel kwani sio maarufu kama vile Harmonize.

View Comments