In Summary

•Karen alichapisha picha inayoonyesha tumbo lake lililochomoza na kuambatanisha na ujumbe wa kimafumbo wa kudokeza kuwa hajabeba ujauzito.

•Licha ya ufafanuzi wake, baadhi ya wanamitandao waliotoa maoni waliendelea kusisitiza kuwa ni mjamzito.

KAREN NYAMU
Image: HISANI

Katika siku za hivi majuzi kumekuwa na madai kuwa seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ni mjamzito. 

Baadhi ya wanamitandao makini ambao waliona picha ambazo wakili huyo alichapisha kwenye kurasa zake hivi majuzi walihukumu tumbo lililochomoza kuwa ujauzito, madai ambayo amejitokeza kukanusha.

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Karen Nyamu alichapisha picha inayoonyesha tumbo lake lililochomoza na kuambatanisha na ujumbe wa kimafumbo wa kudokeza kuwa hajabeba ujauzito.

"Lisemalo lipo na kama halipo basi ni kushiba hahaha aki wewe Mungu," aliandika.

Licha ya ufafanuzi wake, baadhi ya wanamitandao waliotoa maoni waliendelea kusisitiza kuwa ni mjamzito.

Madai ya ujauzito wa Karen yalijiri takriban wiki tatu baada yake kufunga safari ya Marekani ambako mzazi mwenza wake Samidoh alikuwa amekita kambi kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja.

Mama huyo wa watoto watatu alithibitisha ziara yake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Huku yuwes (USA)," aliandika chini ya picha aliyopakia Facebook.

Madai ya kuwa seneta huyo alisafiri hadi Marekani ili kuungana na Samidoh. Wawili hao ambao wana watoto wawili pamoja, Samuel Muchoki Jr na Njeri, wanaaminika kuwa kwenye mahusiano.

Wapelelezi wa mitandaoni waliweza kubaini kuwa wazazi wenza hao huenda walikuwa wakikaa pamoja huku ikidaiwa kuwa hata koti ambayo Karen alikuwa amevaa katika picha moja aliyopakia ni ya mwimbaji huyo.

Karen na Samidoh walikaribisha mtoto wao wa kwanza duniani mwaka wa 2020. Wawili hao walibarikiwa na mtoto mwingine mnamo Februari mwaka huu.

View Comments