In Summary

•Nyamu alithibitisha ni maombi yake kwamba mke mwenza huyo wake siku moja atarudi nyumbani ili wawe familia moja kubwa.

•“Ni maombi yetu pia. Tukue familia moja kubwa," Nyamu alisema.

Edday Nderitu, Karen Nyamu, Samidoh
Image: HISANI

Ni maombi ya Seneta Karen Nyamu kwamba mpenzi wake Samidoh atakuja kuungana tena na familia yake na Edday Nderitu.

Siku ya Jumatatu, seneta huyo maalum wa UDA alithibitisha kwamba ni maombi yake kwamba mwanamke huyo anayedaiwa kuwa mke mwenza wake siku moja atarudi nyumbani ili wawe familia moja kubwa.

Nyamu alikuwa amechapisha nukuu kuhusu kuwasaidia wengine wakati mke huyo wa mzazi mwenzake alipofanywa kuwa mada.

"Kumbuka wakati wowote unapokuwa katika nafasi ya kusaidia mtu, furahiya kufanya hivyo kila wakati kwa sababu huyo ni Mungu anayejibu maombi ya mtu mwingine kupitia wewe," Karen Nyamu aliandika kwenye mtandao wa Facebook siku ya Jumapili.

Shabiki mmoja alijibu, "Siku moja familia ya Edday itaungana tena."

Bila kusita, seneta Nyamu alionekana kukubaliana na maoni ya shabiki huyo na wakati huo akadokeza kwamba angefurahi sana kuona familia ya Muchoki ikiungana na kuwa kubwa tena.

“Ni maombi yetu pia. Tukue familia moja kubwa.”

Katika maoni mengine, shabiki alimuuliza jinsi alivyokuwa akimsaidia mke huyo wa Samidoh kujibu maombi yake.

‘Nashangaa ni maombi gani ya (Edday) ambayo Mungu anajibu kupitia wewe,” Mtumiaji wa Facebook aliuliza.

Karen alijibu, “Mungu atatumia watu wengine kuniamini.

Seneta Nyamu amekuwa akitumia wakati mzuri na mzazi mwenzake, Samidoh katika wiki za hivi majuzi wakati mke wa mwimbaji huyo wa Mugithi akiaminika kuwa Marekani ambapo anafurahiya muda na watoto wake na marafiki wengine.

Katika siku za nyuma Nyamu na Edday wameonyesha waziwazi uhusiano mbaya kati yao huku seneta huyo akikosolewa mara kwa mara kwa madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh, madai ambayo ameyakanusha mara kadhaa.

Mwezi Februari, Bi Edday alimwandikia Samidoh ujumbe mrefu kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimuonya kwamba hayuko tayari kulea watoto wao katika ndoa ya wake wengi. Hii ilikuwa baada ya msanii huyo kuonekana na mzazi mwenzake, Karen Nyamu licha ya awali kudaiwa uhusiano wao umefika mwisho.

Edday alimtaja Bi Nyamu kama mtu asiye na maadili na asiyeheshimu familia yake. Alidokeza kuwa takriban miaka mitatu iliyopita ya ndoa yake imejawa na maumivu na fedheha nyingi. Hata hivyo, alisema licha ya yote amebaki mwaminifu na ameendelea kuunga mkono kazi ya msanii huyo wa nyimbo za Kikuyu. 

"Nimebaki mwaminifu kwako bila kujali kudharauliwa, kudhalilishwa na kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii, umenifanya nionekane mjinga na kuchukulia ukimya wangu kuwa wa kawaida, nimekusaidia kuinua kipaji chako na kukuunga mkono kwa yote, lakini kitu kimoja nimekwambia na nasema hapa tena sitalea watoto wangu katika familia ya wake wengi," alisema kwa uchungu.

Alibainisha kuwa ndoa yake ilikuwa nzuri siku za awali kabla ya mtu wa tatu kuingia ndani yake takriban miaka mitatu iliyopita.

View Comments