In Summary

•Karen Nyamu kwa mara nyingine amebainisha kuwa Bi Edday Nderitu alimwachia mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

•Nyamu alikanusha madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh na ya 'kumuiba' mwimbaji huyo wa  Mugithi kutoka kwa mkewe, Edday Nderitu.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu kwa mara nyingine amebainisha kuwa Bi Edday Nderitu alimwachia mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na drama nyingi maishani alikuwa akijibu madai ya kuwa na mume wa mwanamke mwingine alipotoa ufafanuzi huo.

Huku akijibu moja ya machapisho ya wakili huyo kwenye Facebook, mwanamke mmoja alimwambia, "Na huko na bwana wa wenyewe."

 Karen Nyamu alijibu kwa ujasiri, "Niliwachiwa."

Hii si mara ya kwanza kwa seneta huyo wa chama cha UDA kufafanua kuwa hakuiba mume wa mwanamke mwingine.

Katika mahojiano na Ala C mwezi uliopita, Karen Nyamu alikanusha madai ya kuvunja ndoa ya Samidoh na ya 'kumuiba' mwimbaji huyo wa nyimbo za Mugithi kutoka kwa mkewe wa miaka mingi, Edday Nderitu.

Sijawahi kumuibia mtu mume, tena huyo mwanaume, nina watoto naye na anapenda watoto. Ukitaka kugombana na kutofautiana naye, jaribu kumtenga na watoto wake, wote,” alisema.

Nyamu alidokeza kuwa mzazi mwenzake ameweza kutunza nyumba zake zote mbili, yake na ya Edday Nderitu kwa miaka mingi.

Aidha, seneta huyo wa kuteuliwa alidokeza kwamba licha ya drama zote katika maisha yake ya mahusiano, yeye ni mwanamke mwaminifu sana na huwa anampigania tu Samidoh kwa sababu ni baba wa watoto wake.

Baada ya mahojiano hayo ya Nyamu, Bi Edday Nderitu ambaye anaendelea kufurahia muda na familia yake nchini Marekani alijitokeza kujibu ambapo alibainisha kuwa alimuacha mumewe ili kuwa na mwanamke ambaye alionekana kumtaka zaidi.

"Wacha nifafanue mambo machache ambayo yalishirikiwa mtandaoni na sio sahihi. Siko kwenye ndoa ya wake wengi, kama ilivyoelezwa nilimuacha mume kwa yeyote aliyemhitaji zaidi,” Edday alisema kupitia Facebook.

Aliongeza, "Nilifanya uamuzi wa kujiondoa mimi na watoto wangu kutoka kwa mazingira hayo yenye sumu, haswa binti yangu kijana ambaye kwa bahati mbaya anapokea moja kwa moja tabia isiyoaminika iliyoonyeshwa."

Mama huyo wa watoto watatu alidokeza kuwa hajutii uamuzi wa kugura ndoa yake ya miaka mingi na akaweka wazi kuwa ameweza kuwalea watoto wake bila usaidizi wowote.

Pia alizungumzia madai ya Karen Nyamu kwamba yeye na watoto wake huwa wanawasiliana na mwimbaji Mugithi kwa simu.

"Kuhusu mawasiliano na simu za video, nitaachia hapo kwani baadhi ya watu wanaonekana kuwepo wakati hilo linafanyika lakini mimi sifahamu. Katika msimu huu mpya wa maisha yangu, sihitaji drama yoyote, nahitaji amani tu, natumai kipindi kijacho cha mfululizo huu jina langu litaachwa,” alisema.

View Comments