In Summary

•Nyamu alifichua kuwa video iliyomwonyesha akimnunulia ‘mubaba’ wake pombe ya bei ghali ilikuwa tangazo tu la kibiashara.

•Seneta Nyamu alifichua kuwa mpenzi wake Samidoh hakupenda wazo la yeye kufanya tangazo hilo na alimkaripia kwa hilo.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ameweka wazi kuwa hakuwahi kununua pombe ghali ya Ksh 420,000 kama ilivyodaiwa mwezi uliopita.

Katika mahojiano na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa video iliyomwonyesha akimnunulia ‘mubaba’ wake pombe ya bei ghali ilikuwa tangazo tu la kibiashara.

Karen alifichua kwamba alikuwa akipitia kwenye duka la pombe linalomilikiwa na rafiki yake wa zamani alipoombwa kufanya tangazo hilo kwa nia ya kulipigia debe duka hilo, jambo ambalo hajazoea kufanya.

"Walichukua video kwa kutumia simu yao. Walinitumia video iliyohaririwa ili kuidhinisha na nichapishe kwenye akaunti zangu za Instagram, Twitter na Tiktok ili kutangaza hivyo,” Karen Nyamu alisimulia.

Seneta huyo wa UDA alidai kuwa licha ya kufanya video hiyo ya tangazo hilo kwa hiari, hata hivyo alisita kuichapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kwa vile hakufurahishwa na tabia iliyoonyeshwa.

Alidai kuwa wahudumu wa duka hilo la vileo walitafuta usaidizi wa wanablogu kusambaza video hiyo baada ya kuona hakuwa akiichapisha.

"Sina sifa zilizoonyeshwa kwenye video hiyo, nilikuwa na wasiwasi kuichapisha. Waliniomba nichapishe na wakaona ninasitasita, kwa hivyo wakaingiwa na hofu na kuituma kwa wanablogu baada ya kuona sikuichapisha,” alisema.

Nyamu alisisitiza kuwa yeye si mtu ambaye anapenda kujionyesha licha ya kuwa tajiri kifedha na kuishi maisha mazuri.

Pia alidokeza kuwa hakufurahishwa na jambo la kuonekana akitoa pombe kama zawadi kwa Siku ya kina baba.

"Mimi ni kiongozi, ninayechumbiana naye ni kiongozi wa jamii. Sisi ni kioo kwa jamii. Hatuwezi kuonyesha kuwa zawadi pekee tunayoweza kutoa ni pombe,” alisema.

Alisema baada ya video hiyo kuwekwa hadharani aliwasiliana na wahudumu wa duka hilo la vileo na kuwakaripia kwa kuisambaza. Alisema hata hivyo uharibifu ulikuwa tayari umefanyika na hivyo alilazimika kutumia saa zilizofuata kujitetea na kuwaeleza watu kuwa lilikuwa ni tangazo la kibiashara.

“Sam alikuwa akinilalamikia kwa nini nilifanya tangazo bure ilhali hapo awali nimekuwa nikipewa nafasi nyingi ya kufanya matangazo ya pesa na nimekuwa nikikakataa ofa hizo. Alihoji kwani mtu niliyemfanyia tangazo ni nani kwangu,” Nyamu alisema.

Mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa mwimbaji huyo wa Mugithi hakupenda wazo la yeye kufanya tangazo hilo na alimkaripia kwa hilo.

Pia alifichua kuwa kama ingekuwa kweli alinunua pombe hiyo, baba huyo wa watoto wake wawili wadogo hata hangekubali kamwe zawadi hiyo ya bei ghali kutoka kwake na hata angemwomba arejeshe dukani. 

"Mimi sio mtu wa kughushi mambo. Siwezi kununua pombe ya Ksh 420,000. Mimi sio mjinga, hata ningerudishwa dukani na huyo wanayesema nilikuwa namnunulia," alisema.

Mnamo siku ya akina baba mwezi uliopita, video iliyomuonyesha seneta Nyamu akimnunulia ‘mubaba’ wake pombe ya bei ghali ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia mseto kutoka kwa wanamitandao Wakenya.

View Comments