In Summary

•Rayvanny alichapisha video yake akipiga gumzo na wanaume wawili wanaoaminika kuwasilisha pete hiyo katika ofisi za lebo hiyo.

•Rayvanny aliomba mtu yeyote ambaye angeokota pete hiyo kufanya mipango ya kumrejeshea huku akiahidi kutoa zawadi nono kwake 

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Mwimbaji mashuhuri wa Bongo, Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny ni mtu mwenye furaha baada ya kurudishiwa pete yake ya thamani iliyopotea wiki iliyopita.

Siku ya Alhamisi, Bosi huyo wa Next Level Music alichapisha video yake akipiga gumzo na wanaume wawili wanaoaminika kuwasilisha pete hiyo katika ofisi za lebo hiyo.

Rayvanny ambaye alikuwa ametoa wito kwa yeyote atakayepata pete hiyo kumrudishia aliwashukuru wawili hao na kuwataja kuwa watu wenye roho nzuri.

"Watu wenye roho nzuri bado ni wengi sana. Imagine jamaa wamenirudishia pete yangu iliyopotea Mbagala," aliandika kwenye video aliyochapisha Instagram.

Alieleza furaha yake kubwa iliyosababishwa na kupatikana kwa pete hiyo na kuweka wazi kuwa hawezi kuamini kitendo cha wema cha wanaume hao wawili.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Wikendi iliyopita, Rayvanny alifichua kwamba alipoteza pete yake ya thamani wakati akitumbuiza mjini Mbagala, Tanzania.

Rayvanny alikuwa mmoja wa wasanii walioalikwa kuwaburudisha wageni katika hafla ya Benki ya CRDB siku ya Ijumaa jioni. Alipiga shoo ya kusisimua lakini katika harakati hiyo akapoteza pete yake ya thamani jukwaani.

Baadaye, alitoa ombi maalum kwa mtu yeyote ambaye angeokota pete hiyo kufanya mipango ya kumrejeshea huku akiahidi kutoa zawadi nono kwake 

"Wanangu wa Mbagala nimedondosha pete yangu leo kwenye show ya CRDB," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Rayvanny alimtaka mtu anayeshikilia pete hiyo ambayo alionyesha wazi kuwa ni ya maana sana kwake kuiwasilisha katika ofisi za lebo yake ya NLM.

"Atakayeiokota kuna zawadi nono kwa ajili yake anaweza kuileta NLM au anicheki DM tafadhali," alisema.

Msanii huyo wa zamani wa WCB ni miongoni mwa wanamuziki wa Bongo wanaojulikana kupenda mitindo mizuri na vito vya thamani. Yeye, bosi wake wa zamani Diamond Platnumz, mwenzake wa zamani Harmonize na wengine kadhaa mara nyingi wameonekana wakijigamba na mapambo ya thamani.

View Comments