In Summary

•Malkia huyo wa Bongofleva ameweka wazi kuwa bado hajampata mtu wa kumtoa kwenye maisha ya upweke.

•Wiki jana alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

Zuchu na Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM// ZUCHU

Malkia wa Bongofleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu amesisitiza kuwa hachumbiani na mtu yeyote kwa sasa.

Katika chapisho lake la hivi punde kwenye mtandao wa Instagram, mwimbaji huyo mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni aliweka wazi kuwa bado hajampata mtu wa kumtoa kwenye maisha ya upweke.

"Mie MC wa harusi yangu nishapata, bado Bwana harusi tu," alisema.

Binti huyo wa malkia wa mipasho, Khadija Kopa, alikuwa akimtambua mfawidhi wa harusi ambaye aliwachezea bwana na bibi harusi wimbo wake mpya 'Utaniua' kwenye hafla ya harusi ya hivi majuzi.

Zuchu alionekana kupendezwa na jinsi wenye harusi walicheza wimbo huo vizuri na kuwasihi wengine kuiga mfano wake.

"Utaniua kwa kweli ni wimbo mzuri kwa mchumba wako," alisema.

Wiki iliyopita,  Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yake kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Binti huyo wa Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.

Baadaye, Diamond alizamia kwenye mtandao wa Instagram kuthibitisha kutengana na binti huyo wa Khadija Kopa.

Katika taarifa yake, bosi huyo wa WCB aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena. Alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."

Siku ya Jumanne hata hivyo, alionyesha mahaba makubwa kwa msanii  huyo wake kwa kumnunulia pambo la bei ghali.

Diamond akiwa jijini London, Uingereza alionekana kwenye video akiwa ameshika cheni maridadi ya fedha yenye kichwa cha malkia ambayo alinunua katika duka moja la mapambo jijini humo.

Kulingana na taarifa kwenye ukurasa rasmi wa Wasafi, alinunua cheni hiyo inayomeremeta maalum kwa Zuchu.

"Simba amenunulia Zuchu pambo jipya kabisa jijini London," taarifa hiyo ilisoma.

Wimbo wao 'Mtasubiri' ambao unawasuta wanaochukia uhusiano wao uliambatanishwa na video hiyo.

View Comments