In Summary

• YY Comedian amekanusha uvumi kuwa mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili Alpha Mwana Mtule amefariki dunia.

•B Classic amewaomba Wakenya kumsaidia Mwanamtule huku akidokeza kumekuwa na masuala fulani katika maisha yake hivi majuzi.

Image: INSTAGRAM// ALPHA MWANA MTULE

Mchekeshaji YY Comedian amejitokeza na kukanusha uvumi kuwa mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili Alpha Mwana Mtule amefariki dunia.

Hii ni baada ya tetesi nyingi kuibuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwanamuziki huyo ambaye pia ni mtumbuizaji alifariki kwa kujitoa uhai.

Katika taarifa kwa mashabiki siku ya Alhamisi jioni, YY hata hivyo alithibitisha kuwa Mwana Mtule bado yuko hai.

“Nashukuru Mungu mwanamtule bado yuko hai,” YY Comedian aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Baba huyo wa binti mmoja hata hivyo alifichua kuwa mwanamuziki huyo wa injili kwa bahati mbaya yuko katika hali mahututi.

"Pona haraka kutoka kwa hali hiyo mbaya," YY alisema.

Mwanamuziki mzaliwa wa Pwani, B Classic 006 pia alithibitisha katika taarifa ya video kwamba mwimbaji huyo mwenzake hajafa kama inavyodaiwa.

B Classic alishiriki video yake na wasanii wengine waliomtembelea Mwana Mtule kuchunguza jinsi anaendelea na akatumia fursa hiyo kuwaomba Wakenya waache kusambaza habari za uongo kuhusiana na madai ya kifo cha msanii huyo ambaye anafahamika zaidi kwa kuiga sauti ya mburudishaji DJ Afro.

“Kama mnavyoona tumefika maeneo, Mwanamtule hajakufa mazee ako hai, muache kutrendisha vitu huko. Tafadhali,” B Classic alisema kwenye video hiyo.

Aliongeza, “Tuko na Denzeli hapa tumeconfirm, mwananetu ako hai kabisa na tuko sure atarudi tu kwa game na ubaya sana.”

Mwimbaji huyo kutoka Taita Taveta aliendelea kuwaomba Wakenya kumsaidia Mwanamtule huku akidokeza kuwa kumekuwa na masuala fulani katika maisha yake hivi majuzi.

“Mazee msapotini sana huyu kijana. Ni kama kuna maissues tu mbili tatu zilihappen lakini yuko sawa sasa, tafadhali mpeeni sapoti," alisema.

Wasanii hao walieleza kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili anahitaji ushauri kuhusiana na suala ambalo amekuwa nalo.

View Comments