In Summary

•Dr Ofweneke alimhakikishia Akothee sapoti yake kila wakati akisema haijalishi atafanya harusi ngapi, atakuwepo kila mara kutoa huduma zake za ufawidhi.

•Wakati akijibu ujumbe wa mchekeshaji huyo, Akothee alipendekeza kuwa yuko njiani kumleta mpenzi wake wa nane.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Siku ya Jumatatu, mchekeshaji na mburudishaji maarufu wa Kenya Dr Ofweneke alimkejeli rafiki yake Esther Akoth almaarufu Akothee baada ya kufunguka kuhusu masaibu yake.

Akothee mnamo Jumapili jioni alidokeza kuwa mambo hayajakuwa mazuri kabisa upande wake katika miezi michache iliyopita na kufichua kuwa amekuwa katika mchakato wa kupona. Kufuatia kauli ya mwimbaji huyo, Ofweneke, kama Wakenya wengine wengi, alikisia kwamba chochote ambacho Akothee alikuwa akipitia kinahusiana na ndoa yake na Denis Shweizer almaarufu Omosh ambaye anaonekana kutoweka maishani mwake kwa muda sasa.

Mchekeshaji huyo alimhakikishia Akothee sapoti yake kila wakati akisema kuwa haijalishi atafanya harusi ngapi, atakuwepo kila mara kutoa huduma zake za ufawidhi.

“Babe @akotheekenya, hata ufanye harusi ngapi I will always be there (nitakuwepo)!!!” Dr Ofweneke alisema kupitia Instagram.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha ujumbe wake na video yake akiburudisha wageni wakati wa harusi ya Akothee na Omosh iliyofanywa Aprili mwaka huu.

Aliendelea kumtaka mama huyo wa watoto watano achumbiane na mzungu mwingine na wafanye naye harusi.

“Leta mzungu mwingine nkt!! Lakini lazima nicheke. Haya pia lazima yapite nawe utakuwa sawa,” Ofweneke aliandika.

Wakati akijibu ujumbe wa mchekeshaji huyo, Akothee alipendekeza kwa mzaha kuwa yuko njiani kumleta mpenzi wake wa nane.

"The 8th loading," alisema.

Kumaanisha, “Wa nane anakuja.”

Dr Ofweneke ni mmoja wa marafiki wakubwa wa mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 na mara nyingi huwa anachaguliwa kuwa MC katika hafla zake nyingi, pamoja na harusi iliyofanyika Aprili. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mazungumzo yao ya hivi punde kwenye mtandao wa Instagram yalikuwa ya kutaniana tu.

Akothee pia alicheka wakati mwanamtandao mwingine alipopendekeza kuwa tayari yuko njiani kuelekea kwenye uhusiano mwingine, akihitimisha kwamba tayari ameachana na Omosh.

"Wanawake huwa wanamjua mpenzi wao ajaye wanapokuwa kwenye uhusiano na wewe. Ama nadanganya Akothee? Anyway, nasubiri wa 8,” @gibbcliantosomigo alitoa maoni yake kwenye moja ya machapisho ya mwimbaji huyo.

Alijibu, "NKT" na kuambatanisha jibu lake na emoji za kucheka.

Akothee bado hajathibitisha iwapo suala la kisaikolojia ambalo amepitia linahusiana na ndoa yake. Bado hajathibitisha kama ndoa yake bado iko sawa au tayari ameachana na mume wake wa kizungu. Wakenya wengi hata hivyo tayari wamehitimisha kuwa ndoa hiyo haipo tena.

View Comments