In Summary

•Jalang'o alionyesha ujumbe mrefu kutoka kwa Eli akiomba msamaha kwa uhalifu  huo ambao walifanya mapema mwezi Juni.

•Jalang'o alishindwa kuamua ikiwa kweli anafaa kuwapatia wawili hao nafasi nyingine au la huku akitaja walichokifanya  kama  "usaliti mkubwa."

Mchekeshaji Jalang'o akiwa na wafanyakazi wake wawili waliomwibia
Image: HISANI

Mbunge mteule wa Lang'ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang'o amefichua kuwa wafanyikazi wake wa zamani  aliowaachisha kazi baada ya kumuibia Morrison Litiema na Eli Khumundu wanaomba kurejeshwa kazini.

Akiwa kwenye mahojiano na waandishi wa habari za mitandaoni, Jalang'o alionyesha ujumbe mrefu kutoka kwa Eli akiomba msamaha kwa uhalifu  huo ambao walifanya mapema mwezi Juni.

Katika ujumbe huo, Eli alidai kuwa hakuwa na nia ya kuiba pesa zile na kumhakikishia Jalang'o kuwa hangerudia kosa kama hilo iwapo angekubali kumrejesha kazini.

"Aki naomba msamaha sana na najutia makosa. Mkubwa wangu, nilidanganywa aki, sikuwa na hiyo nia ya wizi. Tumetoka mbali sana, urafiki wetu na undugu isiishie hapo. Tafadhali sana nateseka Bungoma, mheshimiwa naomba tu. Nisaidie tu mkubwa wangu, sitawahi kurudia kosa kama hilo," Ujumbe uliosomwa na mchekeshaji 2mbili ulisoma.

Aliongeza, "Watoto hadi saa hii hawajaingia shule. Niliona kukaa Nairobi bila kazi ni ngumu ilibidi nirudi ushago sir. Hata nyumba bado haijakamilika, madirisha bado hakuna. Mbu zinauma watoto sana. Nihurumie tu mheshimiwa aki. Naomba unisamehe haikuwa kusudi yangu."

Mbunge huyo mteule aliweka wazi kuwa tayari amewasamehe wafanyikazi hao wake wa zamani na kufichua kuwa hata amewahi kukutana nao baada ya tukio hilo lililowashangaza Wakenya wengi.

Hata hata hivyo alishindwa kuamua ikiwa kweli anafaa kuwapatia wawili hao nafasi nyingine au la huku akitaja walichokifanya  kama  "usaliti mkubwa."

"Hakuna kitu ambacho akina Eli hawakuwa nacho. Kama unafanya kazi kwangu basi huchukuliwi kama mfanyikazi. Wewe unakuwa sehemu ya familia. Walinisaliti na sijui nifanye nini," Alisema Jalang'o.

Mchekeshaji huyo alidokeza kuwa pesa ambazo Eli na Litiema waliiba zilikusudiwa kwa madhumuni ya kampeni.

Mapema mwezi Juni Jalang'o alitangaza msako dhidi ya wafanyikazi hao wake wa zamani akidai kuwa walitoweka na familia zao na hata kuzima simu zao  baada ya kuiba pesa kutoka kwa moja ya magari yake.

Alitoa ahadi ya shilingi laki moja kwa yeyote ambaye angepiga ripoti kuhusu walikokuwa wawili hao.

"Ukiwaona tafadhali wasiliana 0722915337 au toa taarifa katika kituo cha polisi kilicho karibu nawe Zawadi ya 100k kwa taarifa yoyote itakayopelekea kukamatwa kwao," Alisema.

View Comments