In Summary

•Akothee alifichua kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakituma ushahidi wake akiwa na Nelly Oaks kwa mumewe na kumuarifu kuwa mkewe anamsaliti kimapenzi.

•Akothee alitangaza sasa ataweka mahusiano yake mbali na mitandao ya kijamii kutokana na mazingira sumu ya majukwaa hayo.

Akothee na mumewe Denis Shweizer wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Kundi la Wakenya hasa wanawake wamekuwa wakituma picha na video za mwimbaji Akothee na aliyekuwa mpenzi wake Nelly Oaks kwa mumewe Denis ‘Omondi’ Shweizer baada ya wawili hao kuonekana pamoja wakati wa hafla ya uzinduzi wa biashara ya binti wa mwimbaji huyo, Vesha Okello wikendi iliyopita

Siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakituma ushahidi wake akiwa na mpenzi huyo wake wa zamani kwa mumewe na kumuarifu kuwa mkewe anamsaliti kimapenzi.

Mwanamuziki huyo aliwakosoa wanawake wanaotuma picha na video hizo na kushangaa kwa nini wengi huwa wanafikiria mapenzi kila wanapoona watu ambao walikuwa pamoja wakikutana tena.

"Kwa hiyo lengo lako ni nini? Unataka akuoe wewe au dada yako? Kwa hivyo nyinyi watu huwa hamuongei au kusema halloo kwa watu ambao mmewahi kuwa nao, mnachofikiria ni wakati watu wawili wa jinsia tofauti wanapokutana, kichwa chenu kimejaa TU ngono na kurudiana,” Akothee alidadisi.

Aliendelea kufichua kwamba mumewe, Bw Shweizer alikuwa tayari ameona picha zake na Nelly Oaks hata kabla hazijachapishwa mitandaoni.

Pia aliwakejeli wale ambao mwanzoni walikuwa na shaka na ndoa yake na kudai kuwa wao ndio wale wale wanaojaribu kuivunja na kuomba kuwa mipango ya kando ya mumewe mzungu.

"Unafikiri mimi ni kama wewe? Nitafichua DMS zenu zote na jumbe zilizotumwa kwa mume wangu. Mlisema hakuna ndoa ni video shoot, sasa mnataka kuwa sehemu ya ndoa, wajinga!” Akothee alisema.

Aliongeza, “Bado nina ndoa yenye furaha na mume wangu wa pekee Omondi Denis, ambaye mlisema nimemuajiri, hana familia wala nyumba, sasa amekuwa muhimu. Wanawake wanamtumia picha wakiomba kuwa side chick.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 wakati huo huo alitangaza kwamba sasa ataweka mahusiano yake mbali na mitandao ya kijamii kutokana na mazingira sumu ya majukwaa hayo.

Niliona baadhi ya watu wakitoa maoni yao kuwa wanapendelea mahusiano yangu ya awali kuliko huu wa sasa, pelekeni maoni yenu benki, tuone kama yanaweza kulipa bili, mimi ndiye niliye kwenye uhusiano, shughulika na yako ambayo ni mbaya.

“Nimeondoa rasmi maisha yangu ya mapenzi kwenye mitandao ya kijamii .Nimejifunza kuwa , jukwaa hili limejaa wivu, uozo, uovu, waliopotea wanaotaka kukuona chini, wasio na furaha, kama sivyo watajaribu kukukasirisha. Takataka!,” alisema.

Katika siku chache zilizopita, kumepamba moto mitandaoni baada ya Akothee na meneja wake Nelly Oaks kuonekana pamoja wakati wa uzinduzi wa biashara ya binti yakeVesha Okello wikendi iliyopita. Baadhi ya wanamitandao wameibua wasiwasi juu ya suala hilo lakini mwimbaji huyo ameshikilia kuwa Nelly atabaki kuwa sehemu ya familia yake milele licha ya kutengana kwao zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

View Comments