In Summary

•Baadhi ya watanzania wamekuwa wakimshambulia Zari kuhusu umri wa mumewe na mwonekano wake hadharani.

•Zari aliwataka mashemeji hao wake wa zamani kusonga mbele na maisha yao akibainisha kuwa tayari miaka 5 imepita tangu aondoke Tanzania.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Katika siku chache zilizopita, mwanasholaiti wa Uganda Zari Hassan na mashemeji wake wa zamani, Watanzania wamekuwa wakibadilishana maneno mitandaoni, mada kuu ikiwa ni mume wake Shakib Cham Lutaaya.

Baadhi ya watanzania watumizi wa mtandao wa Instagram wamekuwa wakimshambulia mzazi mwenza huyo wa staa wa Bongo Diamond Platnumz kuhusu umri wa mume wake na mwonekano wake hadharani.

Baadhi ya wanamitandao  wameibua wasiwasi kuhusu pengo kubwa la umri kati ya wanandoa hao huku wengine wakidai kwamba Shakib anaonekana kutokuwa na furaha wakati akiwa na mama huyo wa watoto watano. Kwa sasa Zari ana umri wa miaka 42 ilhali Shakib alifikisha miaka 31 Desemba mwaka jana.

"Lakini nyie Waafrika, kijana awe mdogo, hana raha au vipi, tatizo lako ni nini? Je,  (Zari) ni wewe?  (Shakib) ni wewe? Waruhusu watu waishi maisha yao kwa njia zao, kwa matakwa yao. Pelekeni hisia huuuko!!" Shabiki mmoja alibainisha kwenye sehemu ya maoni ya chapisho la hivi majuzi la Zari kwenye Instagram.

Huku akikubaliana na maoni ya shabiki huyo, mwanasosholaiti huyo alibainisha, "Sio Waafrika, ni Watanzania!"

Mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 42 alishangaa ni kwa nini Watanzania wanapenda kuibua masuala linapokuja suala la mahusiano yake ilhali hawapati shida ya kukosoa wakati mtu mwingine anafanya jambo sawa.

"Ni Tanzania pekee ambapo ikikuja kwangu, wanaume wa miaka 32 wanachukuliwa kama watoto. Sijawahi kuona watu wabaya kama wao," Zari alisema.

Siku ya Ijumaa, Zari ambaye alionekana kuchoshwa kabisa na raia wa nchi hiyo jirani aliwataka wajali mambo yao wenyewe.

"Watanzania bana.. sijui mdogo, sasa ni mzee. Hacheki, oh leo kafosiwa.. Mmepotoshwa. Yenu ni kuangalia ya watu. Aai, kwa mara moja mjali maisha yenu wenyewe," alimjibu shabiki aliyedai mumewe anaonekana mzee.

Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz aliwataka mashemeji hao wake wa zamani kusonga mbele na maisha yao sasa akibainisha kwamba tayari miaka mitano imepita tangu aondoke Tanzania.

Zari na Shakib walifunga ndoa (Nikah) mnamo Aprili, 16 baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa miezi kadhaa.

View Comments