In Summary

•Diamond alimweleza Zuchu kwanini hakumsherehekea na kumtumia zawadi  siku ya Valentine's kama wanaume wengine.

•Diamond alimhakikishia binti huyo wa malkia wa mipasho, Khadija Kopa, kuhusu mahaba yake mazito kwake.

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Malkia wa Bongo, Zuhura Othman almaarufu Zuchu alishindwa kujizuia baada ya bosi wake na ambaye anaaminika kuwa mpenzi wake pia, Diamond Platnumz kumtumia ujumbe mzuri wa siku ya wapendanao

Katika barua ambayo mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' alionyesha kwenye akaunti yake ya Snapchat, Diamond alimweleza kwanini hakumsherehekea na kumtumia zawadi kochokocho siku ya Valentine's kama jinsi wanaume wengine wengi ulimwenguni kote walivyowafanyia wapenzi wao.

"Kheri ya siku ya wapendanao mpenzi. Ndio, najua unadhani nimechelewa, sijachelewa kwa sababu kwetu kila siku ni siku ya wapendanao. Ndio maana sikutaka kukuletea chochote jana (Februari 14) ili ujue kwamba jana  sio siku tu, ila kwetu kila siku ni siku muhimu," ujumbe wa Diamond ulisoma.

Bosi huyo wa Wasafi aliendelea kumweleza Zuchu jinsi alivyombadilishia mtazamo wake wa siku ya Wapendanao duniani.

Pia alichukua fursa kumhakikishia binti huyo wa malkia wa mipasho, Khadija Kopa, kuhusu mahaba yake mazito kwake.

"Siku ya Valentine’s haikumaanisha chochote kwangu hapo awali. Nataka ujue kwamba nakupenda jana, leo, kesho , kila dakika na kila sekunde ya maisha yetu," 

Diamond zaidi alimuombea mpenzi huyo wake furaha isiyo na kifani na baraka za Mungu tele maishani.

"Mungu ajaze moyo wako furaha na pochi kwa pesa ili uweze kununua ardhi na Nyumba zaidi Zanzibar," aliandika.

Zuchu ambaye alishindwa kabisa kuficha furaha yake alifichua jinsi alivyowezwa na hisia na kuangua kilio cha furaha baada kupokea ujumbe huo mzuri wa mapenzi kutoka kwa anayeusisimua mtima wake.

"Nimelia kama fala. Ataniua," alisema kando ya picha ya barua ya Diamond ambayo alionyesha siku ya Jumatano.

Hivi majuzi, Diamond aliwasisimua wanafamilia wake baada ya kumtambulisha malkia huyo wa Bongo kama mke wake wakati wa karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya dada yake mkubwa Esma Platnumz.

Baada ya kutoa hotuba yake kwenye karamu hiyo, bosi huyo wa WCB alimwalika Zuchu na kumtabulisha kama mwenzake.

"Sasa mwenzangu Zuhura akasema angependa sana tukuje pamoja. Sasa mimi ni shabiki wa maagizo naomba aje awasilishe," Diamond alisema huku chumba cha sherehe kikijawa na shangwe na nderemo.

Kabla ya kuondoka jukwaani na kuchukua nafasi yake, mwimbaji huyo pia alimtaja Zuchu kama  wifi wa dada yake Esma.

"Hapo ndipo tutajua kama ana mapenzi na wifi wake," alisema.

Wahudhuriaji wa karamu hiyo walionekana kufurahishwa sana na utambulisho wa Diamond kwa Zuchu, ishara ya wazi kuwa wengi wao wameidhinisha uhusiano kati ya wawili hao na wapo tayari kushuhudia ndoa.

View Comments