In Summary

•Wanjiru alimsifia mke halisi wa Bw Peter Muriithi almaarufu Mwamba kwa kuwaruhusu kuigiza pamoja kama mke na mume bila kuibua malalamiko.

•Wanjiru alisema alianza kazi ya uigizaji wa vipindi mnamo mwaka wa 1997 baada ya kustaafuu kutoka kazi ya ualimu.

Mwigizaji Elizabeth Wanjiru almaarufu Charity Mwamba
Image: HISANI

Mwigizaji mkongwe Elizabeth Wanjiru almaarufu Charity Mwamba kutokana na kipindi 'Mother- in-Law' amefunguka kuhusu taaluma yake ya uigizaji.

Akiwa kwenye mahojiano na Kamuhunjia, Wanjiru alisema kuwa nafasi ya mama mkwe ambayo ameicheza vyema kwa zaidi ya miaka kumi haionyeshi maisha yake halisi.

Wanjiru ambaye amekuwa akiigiza kama mke wa Bw Mwamba alipuuzilia mbali  mahusiano yoyote ya kimapenzi na mwigizaji huyo mwenzake nje ya kipindi hicho.

Mwigizaji huyo alimsifia sana mke halisi wa Bw Peter Muriithi almaarufu Mwamba kwa kuwaruhusu kuigiza pamoja kama mke na mume bila kuibua malalamiko.

"Inafaa kuwa hivo. Mtu ambaye nashukuru zaidi kwa kufanikisha hilo ni mke wa Mwamba kwa kuwa huwa anamruhusu kufanya hilo," Wanjiru alisema.

Wanjiru alisema kuwa Bi Muriithi amekuwa akichukulia uigizaji wao pamoja kama mtu mzima. Alifichua kuwa miaka yote Mwamba amekuwa mtaalamu sana katika kazi yake na amewapa sababu kuwa ni mtu wa kuaminiwa.

"Kusema kweli yeye ni mtu mzima. Sio mtu wa kutisha ambaye anapuuzilia hisia za mkewe. Nashukuru Bi Muriithi kwa kutupatia Mwamba tuigize naye. Pia nashukuru mume wangu kwa kuniruhusu nicheze nafasi hiyo," Wanjiru alisema.

Wanjiru alisema alianza kazi ya uigizaji wa vipindi mnamo mwaka wa 1997 baada ya kustaafuu kutoka kazi ya ualimu.

View Comments