In Summary

• Mwanahabari mmoja kutoka Tanzania ameibua mjadala mkali kuhusu nani anayepaswa kupewa ubalozi wa kampuni mbalimbali.

• Kulingana naye, watu wengi maarufu wamepata mikataba hiyo ila hawana ushawishi wa kuleta wateja.

Mwanahabari na mwanablogu kutoka huko Tanzania, Fredrick Bundala  ameibua mjadala mkali miongoni mwa mashabiki na washikadau mbalimbali baada ya kuuliza kwamba nani anapaswa kupewa mikataba ya ubalozi kati ya watu maarufu katika mitandao ya kijamaa na wale wenye ushawishi miongoni mwa watu.

Bundala alisema kwamba kuwa na wafuasi wengi haimaanishi mmoja anaweza kuwashawishi watu kununua bidhaa ya kampuni fulani.

Aidha alielezea kisa kimoja ambapo alikosa dili ya ubalozi kwa sababu alikuwa na wafuasi wachache katika mitandao ya kijamii.

"Kuna bosi wa kampuni moja aliniambia wanatoa mikataba ya ubalozi kwa walio na zaidi ya wafuasi milioni moja pekee,"  Fredrick Bundala alisema.

Alikiri kwamba kuna wasanii wengi ambao wana wafuasi kibao katika mitandao ya kijamii ila inawawia vigumu kwa ngoma zao kupata hata views laki tano.

Alizitaka taasisi za kuandaa matangazo na kutoa mikataba ya ubalozi kutafuta mbinu mbadala ya kutambua watu faafu wa kupewa kazi hizo badala ya kufuata upepo wa ubabe katika mitandao ya kijamii.

Kimzaha tu aliwakejeli waliomnyima nafasi hiyo kipindi alikuwa bado ana wafuasi wachache akisema kwamba huenda sasa wakawazia kufanya nao kazi.

"Hata hivyo, tumesalia na wafuasi laki mbili tu kufikia kigezo hicho, labda bosi mkubwa atatusikiliza,"Bundala aliandika.

Mashabiki wake walijitokeza kwenye 'comment section' wakimpa motisha na kuonyesha jinsi wanavyoikubali kazi yake na kumsihi kuzidi kujituma hata zaidi licha ya vikwazo hivyo.

Asilimia kubwa walikubaliana na kauli yake, huku wakitoa ombi kwa kampuni kubadilisha mbinu za kufanikisha mchakato huo.

"Hata wenye wafuasi milioni moja wengi wao ukiangalia kwenye comments zao utakuta meseji kumi tu. Ukifanya utafiti zaidi utakuta hao wafuasi ni wa kughushi tu," shabiki mmoja aliandika.

Wewe una maoni yapi kuhusu kauli hii, na je wahusika watalifanyia kazi na kubadilisha mbinu zao?

 

View Comments