In Summary

•Mavoko aliweka wazi kuwa hakuna hela ambazo aliagizwa kulipa na lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz.

•Pia alisema hakuna vizuizi ambavyo aliwekewa hata kwenye nyimbo alizotengeneza wakati alipokuwa Wasafi.

Rich Mavoko na Bosi wa WCB Diamond Platnumz
Image: HISANI

Mwanamuziki Richard Martin Lusinga almaarufu Rich Mavoko amepuuzilia mbali madai aliagizwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha wakati alikatisha mkataba wake na WCB.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Mavoko aliweka wazi kuwa hakuna hela ambazo aliagizwa kulipa na lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz.

"Mimi sijawahi kuambiwa nilipe hela. Pia sijawahi kulipa hela na sijawahi kufikia kwenye kulipa hela. Ndio maana siwezi kuongelea chochote," Mavoko alisema.

Mwanamuziki huyo kutoka nchi jirani ya Tanzania alisema habari kuwa alilazimika kulipa kitita kikubwa cha pesa ili kuafikia makubaliano ya kukatiza mkataba na WCB ni "maneno ya udaku."

Pia alisema hakuna vizuizi ambavyo aliwekewa hata kwenye nyimbo alizotengeneza wakati alipokuwa Wasafi.

"Kila kitu changu ni cha kwangu. Sijawahi kusimamishwa kutumbuiza. Sijawahi kuambiwa usifanye hiki. Kila kitu ambacho nimeimba nimeandika mwenyewe, sio wasafi ama mtu yeyote, ni mimi na talanta yangu. Hakuna mtu ambaye anaweza kunizuia kuimba wimbo wowote," Alisema.

Vilevile Mavoko ambaye hivi majuzi ameachia albamu mpya 'Fundi' alidai kuwa lebo ya Wasafi haikuwahi kugharamia video ya wimbo wake wowote.

Mavoko aligura Wasafi takriban miaka minne iliyopita. Uvumi ulitanda kuwa aliagizwa kulipa mamilioni ya pesa ambazo hakuwa nazo kwa wakati huo. 

Ripoti mbalimbali zilidai kuwa Baraza la Sanaa nchini Tanzania (BASATA) ndilo lililomsaidia msanii huyo kulipa hela alizodaiwa.

Bosi wa Kondegang Music Worlwide Harmonize ni miongoni mwa wasanii wengine ambao waliwahi kugura Wasafi.

Mwaka jana Konde Boy alidai lebo ya Wasafi ilimwagiza kulipa Tsh500M ili kukubali kukatiza mkataba wake.

View Comments