In Summary

• "Hakuna mtu atakutunza jinsi unavyotaka, lazima ujiwekee viwango kwanza,” aliandika Akothee.

Msanii na mjasiriamali Akothee
Image: Instagram

mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee ameshauri wafuasi wake kujitaka kuridhisha kila mtu na badala yake kuwa wachoyo ili kujiridhisha wenyewe.

Akiachia ushauri uliokolea kupitia Instagram yake, Akothee alipakia picha yake ya kitambo huku akisema kwamba kipindi hicho ambacho ni mwaka 2018 alikuwa ananyong’onyea kutokana na shinikizo kali kutoka kwa wafanyikazi wake pamoja na watu wa karibu naye.

Alisema alilazimika kufanya maamuzi magumu kisha kuanza safari ya matumaini pindi alipogundua kwamba anawafurahisha watu wengi bure na kujipata anaumia mwenyewe, kwa maana hiyo aliamua kufungia watu wengine nje ya mduara wa urafiki wake ili kupata amani ya nafsi.

“Unaweza kufikiria unahitaji watu wengi karibu nawe ili kurahisisha kazi yako, lakini basi hii ni kuchimba shimo kwenye ubongo wako. Nimekuwa na shida sana kwenye safari hii kama mwanamke ili kujaribu kusawazisha,” aliandika Akothee.

Mwanamuziki huyo alizidi mbele kuelezea hatua Madhubuti alizozichukuwa ili kujinasua kutoka kwa shinikizo hilo ambalo alilitaja kuwa lilikuwa linampa taabu sana, haswa katika afya yake ya kiakili.

Hatua ya kwanza kabisa aliyoichukua ni kujitathmini mwenyewe na kujua ni nini haswa kilichokuwa kinampa taabu na kisha kuanza kupotezea baadhi ya mambo na vitu ambavyo havikuwa vinaleta tija katika mzunguko wa maisha yake.

Vile vile Akothee alisema alijiuliza kama kweli ana furaha na kile alichokuwa anakifanya na pia kujitathmini kama kweli anaishi maisha ya kikweli ama anakufa angali hai.

Kando na hayo, pia Akothee alijitathmini kuhusiana na watu ambao alikuwa anaschukua muda mwingi kushinda nao kama kweli wana tija maishani mwake ama ni mzigo tu ambapo pia alijihoji kama angepata matatizo ya kifedha wangeweza kumpa msaada ama ni wale wa kusimama kwenye pembe za chaki na kumcheka kichini chini.

Mfanyibiashara huyo nguli alizidi kwa kutoa ushauri kwa wafuasi wake kwamba katu wasiogope kuwa peke yao hata bila familia kwa sababu muda mwingine mtu anakuwa vizuri akiwa miongoni mwa watu asiowajua kuliko kuwa na watu wa ukoo ambao hawana msaada wowote zaidi ya kejeli tu.

“USIOGOPE KUWA PEKE YAKO hata bila familia, wewe ni bora kuwa na wageni kuliko kuwa na watu wa karibu na wewe ambao wanakunywa maji hadi kaburini. Kuwa mbinafsi na kujijali mwenyewe. Hakuna mtu atakutunza jinsi unavyotaka, lazima ujiwekee viwango kwanza,” aliandika Akothee.

View Comments