In Summary

•Mbosso amesema amekuwa akimtembelea daktari wake mara kwa mara na kuyafuata maagizo yake  katika juhudi za kupona kikamilifu.

•Mbosso alikiri kuwa kupenda nyama kwake kumefanya ashindwe kuyafuata maagizo ya daktari wake kikamilifu.

Mbosso
Image: HISANI

Staa wa Bongo Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso amefichua kuwa anaendelea vyema na matibabu ya tatizo lake la moyo.

Mbosso amesema amekuwa akimtembelea daktari wake mara kwa mara na kuyafuata maagizo yake  katika juhudi za kupona kikamilifu.

"Najitahidi sana kufanya mazoezi. Mi na daktari wangu tunakutana sana mara kwa mara. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo nahitajika nisikule japokuwa uchu unanitesa sana," Mbosso alisema katika mahojiano na Wasafi Media.

Mwanamuziki huyo alifichua kuwa daktari wake amemwagiza kutokula nyama zozote nyekundu na kula zile nyeupe pekee.

"Natakiwa nile samaki, kuku na mboga za majani," Alisema.

Mbosso hata hivyo alikiri kuwa kupenda nyama kwake kumefanya ashindwe kuyafuata maagizo ya daktari wake kikamilifu.

"Kusema ukweli nisiwe mnafiki, najiiba sana. Nyama huwa nagonga wakati mwingine. Nyama kuachana nayo huwa mtiti sana," Alisema.

Staa huyo wa Bongo alisisitiza kuwa amekuwa akiisha na tatizo hilo la moyo na la kutetemeka tangu enzi za kuzaliwa kwake.

Alieleza kwamba  aliamua kufuatilia matatizo yake na kutafuta matibabu baada ya kuwa mtu mzima.

"Mwanzoni nilikuwa naamini ni vitu vya kuridhi kwa sababu  nyumbani kwetu niko na shangazi yangu alipata tatizo hilo kwenye shingo. Niliamini ni ishu za kifamilia,"  Alisema.

Mbosso alifichua kuwa aligundulika kuwa na tatizo la mtiririko wa damu mwilini mwake lililosababishwa na kuzibwa kwa mishipa yake. 

"Tatizo langu ni la mafuta. Mishipa yangu ya damu imezibwa na mafuta. Kwa hiyo damu haizunguki vizuri kwenye mwili. Wakati mwingine nikilala usiku napata maumivu makali kwenye upande wangu wa kushoto. Hadi nalia wakati mwingine," Alisema.

Pia alieleza kuwa tatizo hilo la moyo ndilo linalosababisha mkono wake kushinda ukitetemeka mara nyingi.

 "Maendeleo yangu sio mabaya. Naendelea vizuri, najitahidi kuzingatia ninayoambiwa" Alisema

Katika mahojiano ya awali mwimbaji huyo alifichua kuwa madaktari waliwahi kumwarifu kuwa ugonjwa wake huenda ukamsababishia utasa baada ya kutimiza miaka 30.

"Daktari aliniambia shida yangu huenda ikawa kubwa zaidi  baada ya kufikisha miaka 30. Alisema huenda ikanipelekea nisipate tena watoto nisipofanya matibabu," .

Mbosso alisema aliamua kuwafichulia mashabiki wake kuhusu tatizo lake la moyo ili "wasije wakasikia Mbosso kaanguka ghafla washangae vipi."

View Comments