In Summary

•Kokoto alifichua kuwa ugonjwa wa mwanawe uligunduliwa alipokuwa na umri wa miezi 8 tu baada ya kufanyiwa vipimo vingi. 

•Alisema hali ya mwanawe imemchosha yeye na mkewe kihisia, kisaikolojia na hata kuwanyima usingizi kwani huwa wanatumia wakati mwingi kumshughulikia.

•Pia alifichua kuwa kwa sasa mwanawe amelazwa katika hospitali ya Kenyatta kwa ajili ya matibabu maalum.

Image: FACEBOOK// KOKOTO LIJODI

Muigizaji Kokoto Lijodi anatazamia kuchangisha takriban shilingi milioni 2.5 ili kumpeleka mtoto wake mgonjwa kwa matibabu maalum nchini India.

Mtoto wa kwanza wa muigizaji huyo wa zamani wa Vioja Mahakamani, Wesley, amekuwa akipambana na anemia ya seli mundu kwa takriban miaka 13.

"Wakati ugonjwa ulikuwa ukianza mtoto alikuwa analia sana. Ukiangalia kwenye  viganja vya mikono na miguu yake ungegundua kuwa imefura. Sikuwa najua nini kilichokuwa kinaendelea. Lakini alikuwa analia sana mpaka majirani wanakuja kunigongea mlango. Uchungu ambao mtoto alikuwa akihisi ndio ulifanya alie hivo na hakuwa na uwezo kusema ni wapi alikuwa anaumwa," alisimulia katika mahojiano na Plug TV.

Kokoto alifichua kuwa ugonjwa wa mwanawe uligunduliwa alipokuwa na umri wa miezi 8 tu baada ya kufanyiwa vipimo vingi. Aliongeza kuwa hali ya mtoto huyo imemchosha yeye na mkewe kihisia, kisaikolojia na hata kuwanyima usingizi kwani huwa wanatumia wakati mwingi kumshughulikia.

"Sisi tukifika nyumbani tunakuwa kama walinzi. Kuna wakati mimi huwa katika zamu na wakati mwingine mke wangu. Wakati mwingine sisi hukaa chini tu tunamuangalia kwa sababu ni uchungu ambao hatuwezi kufanyia chochote," alisema.

Muigizaji huyo alibainisha kuwa ugonjwa wa Wesley ni wa ukoo na huenda alirithi kutoka kwa familia yake au upande wa mkewe.

Alifichua kuwa kwa sasa mwanawe amelazwa katika hospitali ya Kenyatta kwa ajili ya matibabu maalum na kudokeza kuwa madaktari wamempatia ushauri kuhusu njia mbili za kutafuta suluhu ya hali hiyo.

Hata hivyo, ameeleza  wasiwasi wake kuhusu njia rahisi ambayo haitatoa suluhisho kamili na hivyo amechagua njia ya pili ambayo ni kumpeleka mwanawe India kwa matibabu maalum. Kokoto anaamini kwamba mara baada ya Wesley kutibiwa nchini India ataweza kuishi maisha ya kawaida licha ya kubeba ugonjwa huo.

"Mahali hali ya mtoto huyo imefika, nilikuwa naomba kama tu tunaweza kuchanga  tumpeleka India kutibiwa. Ukifanya hesabu yote; ujumuishe matibabu, kukaa huko miezi tatu tukisubiri apone,  akirudi pia kuna madawa atahitaji kunywa kama miezi sita hivi, hiyo hesabu yote inakuja takriban milioni 2.5," alisema.

Kokoto anajulikana sana kutokana na kipindi cha Vioja Mahakamani. Kando na Vioja mahakamani, pia ameigiza kwenye vipindi kadhaa vya vichekesho kama vile Hulabaloo.

View Comments