In Summary

• Ikumbukwe miezi michache iliyopita Sonko alituma timu yake kumuendea Achienga baada ya picha yake kusamba mitandaoni ikimuonesha katika hali ya kutia huruma.

Sonko amlisha Achieng keki siku yake ya kuzaliwa
Image: Instagram

Mwanabondia wa kike maarufu nchini Kenya Conjestina Achieng alijawa na furaha baada ya wasamaria wema kujiunga naye siku ya mashujaa Oktoba 20 kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo alikuwa anafikisha miaka 45.

Kundi hio la wahisani ambalo lilikuwa linaongozwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko walimrushia bonge la ‘surprise’ Conjestina na kumfanya ajihisi kama shujaa wa taifa hili, japo kwa muda mrefu wengi wamekuwa wakiteta kwamba alisahaulika licha ya jitihada zake kulibeba jina la taifa mabegani katika mashindani mbalimbali ya ngumi.

Sonko alipakia picha za furaha wakiwa wanamlisha Achieng keki huku akisema kwamba walishiriki naye vitu vingi pamoja na wanawake kutoka kituo cha kurekebisha tabia cha kina mama jijini Mombasa.

“Tuliadhimisha siku ya mashujaa kwa mtindo kwa kujiunga na mmoja wa mashujaa wetu Conjestina Achieng kwa kutimiza miaka 45. Hii pia ilitupa fursa ya kushiriki nyakati za furaha za siku kwa chakula cha mchana, vinywaji baridi, kukata keki, kucheza na kujiburudisha na kila mtu katika kituo cha kurekebisha tabia cha Mombasa Women,” Sonko aliandika.

“Heri ya kuzaliwa shujaa Conjestina na Mashujaa yenye furaha kwetu sote, tunaojitahidi kuwa mashujaa kwa njia zetu tofauti kila siku!” Sonko aliongezea.

Ikumbukwe miezi michache iliyopita paliibuka na taarifa zisizo za kufurahishwa kwamba mama huyo wa mtoto mmoja alikuwa ameathirika tena kiakili baada ya picha yake ya kutia huruma kusambazwa mitandaoni.

Sonko alijitolea na kutuma timu yake kumuendea ili kumuokoa ambapo walimchukua katika kituo cha kurekebisha tabia cha Mombasa ambapo amekuwa akipatiwa matibabu ya kiakili.

 

View Comments