In Summary

• Orodha hii inawajumuisha wasanii kutoka mataifa ya Kenya na Tanzania ambapo ushindani wa muziki unasemekana kuwa juu na wasanii wengi kila uchao kuibuka.

Baadhi ya wasanii waliojikuta kwenye kashfa ya kuiba ngoma za wenyewe
Image: Instagram

Kufuatia sakata la msanii Zuchu kudaiwa kuiba baadhi ya vipengele kweney wimbo wa msanii mwenziwe kutoka tasnia ya Injili, Tanzania, Radiojambo.co.ke imetambua kwamba msanii huyo si wa kwanza kujipata katika mwanga huo wa kutishia taaluma yake ya kimuziki.

Hapa tunakuandalia orodha ya baadhi ya wasanii kutoka Kenya na Tanzania ambao wamewahi jipata katika gumzo la kudaiwa kufanya wizi wa kazi za wasanii wenzao.

Zuchu

Malkia huyo wa Bongo Fleva amekuwa akifanya vizuri tangu kutambulishwa rasmi kwenye lebo ya WCB Wasafi. Wikendi iliyopita ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kujipata katika kupakwa tope kwamba ameiba wimbo wa injili.

Inadaiwa kwamba msanii wa injili, Enock Jonas amechukua hatua za kisheria baada ya kudai kwamba Zuchu aliiba kibwagizo na hata staili ya wimbo wake wa ‘Wema wa Mungu’ na kuimba katika kibao chake kipya cha ‘Kwikwi’

Jonas anadai kufidiwa takribani milioni 25 za Kenya sawa na milioni 500 za Kitanzania kwa hatua hiyo ambayo anasema ni kuibiwa wimbo wake, unaojulikana kwa kibwagizo cha ‘Zunguka’

Diamond Platnumz

Mfalme huyo ambaye ameteka Sanaa ya muziki Afrika Mashariki kwa zaidi ya miaka 10 naye hajasazwa katika madai ya kuiba baadhi ya kazi za muziki kutoka kwa wasanii wenzao.

Miaka kadhaa iliyopita wakati yeye na timu yake ya Wasafi waliimba kibao kilichovuma cha ‘Zilipendwa’ msanii mkongwe H-Baba aliibuka na kudai kwamba wazo la kibao hicho lilikuwa lake.

H-Baba aliteta vikali kwamba Diamond alichukua kibao hicho kipindi wakiwa pamoja katika lebo ya Shawarbaru.

Pia mwaka huu Diamond alisutwa vikali kwa kile mashabiki wa muziki walisema aliiba ‘beats’ za ngoma ya Otile Brown ‘Such Kinda Love’ na kuzitumia katika kibao chake cha ‘Naanzaje’

Harmonize

Mwamba huyu hapa pia naye hajakwepa shoka la tuhuma za wizi wa ngoma za wasanii wenzake.

Wimbo wake wa ‘Amina’ ambao alitoa mwaka jana ulifutwa kwenye mtandao wa YouTube baada ya msanii wa kutema mistari, Rosa Ree kudai kwamba ni wimbo wake na alichukua staili yake katika kufanya wimbo huo.

Bahati na Otile Brown

Hawa pia walijipata pabaya baada ya mashabiki kuwazomea vikali walipogundua kwamab midundo ya collabo yao ya ‘Je Unanifikiria’ ilikuwa imefanana moja kwa moja na wimbo wa Marioo ‘For You’ wawili hao si tu waliiba midundo lakini pia Bahati alisikika akiimba maneno sawa na yale ambayo yanasikika kwenye wimbo wa Marioo.

Khaligraph

Msanii huyo nguli wa kuchana mistari pia amejipata katika joto la kutuhumiwa kuiba miradi kadhaa ya ngoma za wasanii nchini Kenya. Mapema mwaka huu, kundi la Sailors Gang liliibua madai kwamba OG, kama ambavyo anajulikana kimajazi aliiba wimbo wa ‘Kwenda’ ambao walisema ulikuwa wao.

Pia kundi la Buruklyn Boyz lilimshtumu Jones kwa kuchukua maneno ambayo waliyaasisi ya ‘Nikwa ni Shoke’ na kutoa ngoma nayo pasi kuwataarifu.

Bahati na Nadia Mukami

Msanii Bahati pia alitoa ngoma yake na malkia Nadia Mukami, ‘Pete Yangu’ ambayo ilipata pingamizi kubwa kutoka kwa wanamitandao waliwatuhumu wawili hao kwa kuchukua wimbo wa msanii kutoka Rwanda, Butere Knowles mwenye wimbo ‘Peke Yangu’

Nameless

Mnamo 2008, alishtakiwa kwa kuiba beats zilizotumiwa katika wimbo wake. Madai hayo yalitolewa na Serge Nkurunzinza mwimbaji wa Burundi kwa kutumia beat yake kwa wimbo ‘Amahera’. Nameless alikanusha madai hayo akisema mashairi yalikuwa tofauti ingawa beat ilikuwa sawa kutokana na kuchanganyikiwa studio. Nameless alisema amenunua beat hiyo kutoka kwa produsa kutoka Uganda Washington.

King Kaka

Alishutumiwa na ‘Safari Sound Band’ kwa kuiba sehemu ya wimbo mmoja wa bendi hiyo, ambayo aliitumia kwenye wimbo wake.

King Kaka alipuuzilia mbali madai hayo akidai kuwa alikuwa na baraka kutoka kwa mmoja wa wanamuziki nguli wa bendi hiyo.

Weezdom

Msanii huyo ambaye alikuwa wa injili kabla ya kubadilisha na kuanza kuimba nyimbo za kidunia pia mwaka huu alijipata pabaya baada ya kudaiwa kuiba wimbo wa Diana B ‘Mubaba’ ngoma aliyoipa jina ‘Wazae’

View Comments