In Summary

• Miaka miwili iliyopita Nasenya alisema kuwa ili akutangazie biashara yako kwenye kurasa zake mitandaoni, ni sharti utoe kiasi cha laki moja kwa kila chapisho.

Wanawake wenye rate cards za kustaajabisha Kenya
Image: Instagram

Mrithi wa kampuni ya kutengeneza mvinyo ya Keroche, Anerlisa Muigai wikendi iliyopita aligonga vichwa vya habari baada ya kuachia kadi ya kukadiria viwango vyake kwa wanaotaka kutangaza biashara zao kupitia mitandao yake ya kijamii.

Muigai alizindua bei zake ambazo ni ghali mno, jambo lililowavutia watu mitandaoni kuzungumzia hilo.

Katika maelezo ya kina ambayo Muigai aliyaweka kwenye Instastories zake, alisema anatoza kiasi cha dola elfu sita kwa wiki tatu kama mtu anataka biashara yake itangazwe kwenye ukurasa wake rami.

Aliwaambia wale wanaotaka awe balozi wao wa mauzo kuwa watahitaji kuzama mfukoni na kuibuka na kiasi cha dola laki moja ambazo ni sawa na milioni 12 na ushee pesa za Kenya ili kuzipata huduma zake kwa miezi mitatu tu!

Tangazo hili lilipokelewa kwa njia tofauti kutoka kwa wanamitandao ambao waligawanyika kwa maoni, baadhi wakimtetea na wengine wakimuapiza kwa kujiweka ghali kuzidi maelezo.

Lakini je, Arnelisa Muigai ndiye Mkenya wa kwanza kujipata katika ukakasi huu baada ya kutangaza viwango vyake kwa watu wanaotaka kutangaziwa biashara? Bila shaka hapana, hawa pia ni baadhi ya wanawake Kenya waliojipata katika hali kama hii baada ya kutangaza viwango vyao kwa bei.

Azziad Nasenya

Azziad ana umri wa miaka 22 na alipata umaarufu baada ya video ya TikTok yake akicheza ngoma ya Femi One na Mejja ‘Utawezana’ kusambaa mitandaoni. Nasenya alijipata katika gumzo kubwa baada ya kudai kuwa anatoza kiasi cha laki moja kwa kila chapisho ambalo mtu atataka kupakia kwenye mitandao yake ya kijamii.

Nasenya alisema kwa mwezi mtu atahitaji kutoa kiasi cha nusu milioni ili kupata biashara yake kutangazwa katika kurasa za mitandao ya kijamii ya Nasenya.

Manzi wa Kibera

Huyu ni mwanamitindo kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi ambaye pia aliwashangaza wengi alipotangaza bei yake kwa kutoa huduma za mapenzi kwa wanaume.

Alisema kwamba mwanaume ambaye atahitaji huduma za mapenzi kutoka kwake kwa usiku mmoja tu atalazimika kutoa kiasi cha milioni 1.5 pesa za Kenya huku pia akisema wale wanaotaka atokee kwa klabu kutoa laki moja.

View Comments