In Summary

• Ukienda kwenye stori zangu ninazoweka kwenye Instagram, utakuta nyimbo hizi ndizo nyingi ambazo huwa naziweka - Olunga.

Olunga afichua ngoma za Wakenya anazozisikiliza
Image: Instagram

Mshambuliaji matata wa Harambee Stars Michael Olunga amefunguka kuwa kila mara kabla ya kuingia uwanjani kuitumikia timu yake ya Al Duhail inayoshiriki ligi kuu nchini Qatar, huwa aghalabu anasikiliza nyimbo za wasanii Wakenya.

Mwanasoka huyo alifichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa muziki wa Kenya na hata akataja baadhi ya mastaa ambao anawafagilia sana.

Alisema nyimbo anazozipenda zaidi ni nyimbo kutoka kwa mastaa wa Kenya kama Sauti Sol na kikundi cha Hip-hop Wakadinali.

Mshambulizi huyo Mkenya mwenye umri wa miaka 28 alisema pia ana uhusiano mkubwa na Wakadinali tangu alipoenda shule na baadhi ya wanakikundi.

Kundi la Wakadinali limekuwa kwenye vichwa vya habari kwa takriban miaka saba, likitawala mawimbi ya Kenya kuhusiana na muziki wa rap. Ni kikundi  kinachoundwa na Scar Mkadinali, Domani Munga, na Sewer Sydaa.

Akizungumza na Nairobi News kwa njia ya kipekee Ijumaa, Eng Olunga alisema kuwa anawafahamu wanakikundi hao na hata kufichua kuwa alisoma shule moja na Scar ambaye ni mmoja wa kikundi hicho cha rap.

 “Ninawafahamu Wakadinali kwa sababu tulisoma na Scar. Kwa hiyo alikuwa akirap shuleni, na ninakumbuka akiimba hata alipokuwa shuleni.” Olunga alisema.

Kwa kushangaza, mchezaji wa soka anajua orodha nzima ya kucheza ya kundi la Wakadinali.

Alisema kila anapokuwa karibu huwa anapata muda wa kuzungumza na Scar ambaye anaendelea kumsasisha katika albamu inayofuata kwa sababu ni miongoni mwa mashabiki wa kwanza kusikiliza nyimbo zao mpya.

"Siku zote mimi ni miongoni mwa wa kwanza kusikiliza nyimbo zao, ambazo ni mzuri. Nashukuru. Ukienda kwenye stori zangu ninazoweka kwenye Instagram, utakuta nyimbo hizi ndizo nyingi ambazo huwa naziweka”

Mwanasoka huyo aliongeza kuwa kwa kawaida hujaribu kuunga mkono vipaji vya wakenya kadiri awezavyo.

Aliongeza kuwa kwa urithi wake, angependa kukumbukwa kama mtu aliyechangia sio tu katika mpira wa miguu lakini pia kama mwanasoka aliyejifunza vizuri.

"Ningependa kuacha alama sio tu ndani ya uwanja, lakini pia nje ya uwanja."

View Comments