In Summary

• Rapa hao wakongwe hapo zamani walikuwa marafiki wa karibu sana walipoanza kazi zao za muziki.

Redsan, Jua Cali, Nonini
Image: Instagram

Msanii mkongwe wa miziki ya Genge nchini Kenya, Jua Cali kwa mara ya kwanza amezungumzia uhusiano wake na baadhi ya wasanii walioanza gemu la muziki pamoja na ambao kwa sasa hawako ilhali yeye bado ni moto pasi katika sekta ya muziki wa kizazi kipya.

Msanii huyo aliyekuwa na mazungumzo ya kipekee na mchekeshaji Dr Ofweneke kwenye runinga moja humu nchini alifutilia mbali uvumi unaomhusisha kuwa na bifu na msanii ambaye walikuwa wandani sana enzi hizo, Nonini.

Rapa hao wakongwe hapo zamani walikuwa marafiki wa karibu sana walipoanza kazi zao za muziki. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, wanaonekana kutofautiana, na kusababisha uvumi wa uwezekano wa kuwa na uhasama fulani.

Jua Cali alikanusha madai ya kuwepo kwa uhasama baina yake na Nonini na kusema kwamba wakati mwingine maisha hutenganisha watu lakini hilo halimaanishi kuwa ni maadui.

Aidha, alikubali kwamba uhusiano wake na Nonini katika miaka ya hivi karibuni haupo na afya kama ulivyokuwa miaka ya nyuma enzi Genge ndio aina ya muziki uliokuwa gumzo la mjini mpaka kijijini.

"Tuliachana lakini hatukutengana. Maisha yalitokea na yametutengwa kwa muda sasa. Bila shaka tulivyokuwa zamani si kama tulivyo sasa, lakini hata hivyo bado tunazungumza vizuri sana.” alisisitiza Jua Cali.

"Unajua mtu anapoanza kujihusisha na mambo mengine (kando na muziki) au tuseme anaamua kutengeneza njia tofauti, kwa kawaida nyote mtatofautiana." aliongeza.

Jua Cali pia aligusia urafiki wake na mkongwe wa dancehall Redsan. Wawili hao wanasalia karibu sana, alisema, ingawa hawajawahi kufikiria collabo.

Alipoulizwa ni kwa nini hawajawahi kufanya collabo pamoja licha ya ukaribu wao, Jua Cali alisisitiza kwamba hata yeye kwa kweli hajui na kuahidi kumtafuta mkongwe huyo wa Dancehall ili kuona kama watalifanikisha hilo kwa faida ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiuliza swali hilo.

“Kusema kweli siwezi kueleza hilo. Sijui kwa nini hatujawahi kufanya wimbo. Nadhani itabidi nimuulize Redsan kwa nini hatujawahi kufanya jambo pamoja, labda anaweza kuwa na jibu bora zaidi.”

 

View Comments