In Summary

• Alisema podcast yake itaenda hewani kweney mitandao yake ya kijamii kuanzia Alhamisi ya Desemba 15.

• Hatua hii inakuja wiki moja tu baada ya kibarua chake kuota nyasi katika kituo cha runinga cha NTV.

Mwanahabari Mark Masai
Image: FaCEBOOK

Mwanahabari wa muda mrefu, Mark Masai baada ya kufutwa kazi katika kituo cha runinga cha NTV wiki moja iliyopita, amejikusanya na kuanzisha podcast yake mwenyewe mitandaoni.

Masai alikuwa amefanya kazi kama mwanahabari katika runinga hiyo kwa miaka 14 na wengi walimtaja kama moja ya talanta nzuri kwa muda huo wote.

Kuondoka kwake kama kawaida hakukuwa kwa kimya kimya bali kuliibua mawimbi na minong’ono mbalimbali mitandaoni, baadhi wakizua za ndani kuwa kibarua chake kiliota nyasi baada ya uhusiano wake na HR mwanamke katika kampuni ya NMG kuzorota – madai ambayo hata hivyo Masai aliyapinga vikali na kusema angetoa sababu na mwelekeo wake hivi karibuni.

Mwelekeo wenyewe ni kama ndio huo sasa ambao ameutoa – kuanzisha podcast ambayo ameipa jina ‘The Social Newsroom’ na kusema kuwa uamuzi wake ulichochewa na mwelekeo wa kimitandao zaidi na ujio wa dijitali.

“Mabibi na Mabwana: Hapa ni kwetu! Kwa njia mpya ya kufanya mambo. Ili kupata maana katika yale tunayopitia. Ili kupata hadithi ambazo ni muhimu kwetu. Karibu kwa mwelekeo wa mustakabali. #TheSocialNewsoom na @semaboxAfrica Tiririsha Alhamisi hii saa kumi na mbili jioni kwenye mitandao yangu ya kijamii. Kama kawaida, Sambaza, mwambie rafiki!” Masai aliandika.

Wengi walimpongeza kwa kutopoteza muda kujisahau kwa kufutwa kazi na kumkaribisha kwa kuendeleza mambo yake kwa njia za kimitandao zaidi.

“Karibu kwa upande huu mwingine wa kufanya mabo bila kuzuiwa, kila la kheri Mark,” mwanahabari wa upekuzi John Allan Namu alimwambia.

“Ingependeza wakati Masai atapata mafanikio makubwa kwenye jukwaa lake. Labda ni vyombo vya habari vya kawaida ambavyo vimekufa,” mwingine alisema.

View Comments