In Summary

• Omondi alisema uongozi wa Stevo ulimuangusha kwani ndio walishindwa kulainisha mambo kabla ya msanii wao kuelekea Mombasa.

• Omondi ndio alikuwa MC katika tamasha hilo ambapo alitaarifiwa kuwa Stevo hakuwa amelipwa mwisho wa shoo.

Omondi amwazomea uongozi wa Stevo
Image: Instagram

Mchekeshaji Eric Omondi ameutaka uongozi wa kazi za Sanaa za msanii Stevo Simple Boy kujiuzulu mara moja kwa kile alitaja kama ni utepetevu kazini.

Msanii Simple Boy alikuwa mmoja wa wasanii ambao wangetumbuiza katika tamasha la ‘So Fire Fiesta’ liilofanyika jijini Mombasa siku mbili zilizopita kando na msanii kutoka Nigeria, Ruger.

Lakini wengi wa mashabiki wa msanii huyo walipogwa na butwaa wakati msanii Simple Boy alifeli kutumbuiza.

Msanii huyo Alhamisi mchana alitoa taarifa ya kuomba msamaha kwa mashabiki wake waliochukia baada ya kitendo chake kugoma kuingia ukumbini. Alisema kuwa sababu yake kutotumbuiza ilikuwa ni ukiukwaji wa maelewano na mapromota wa shoo ile ambao walitaka kumzunguluka afanye shoo bila malipo.

Omondi sasa anailaumu ‘management’ ya Stevo akisema kuwa ndio walimfeli kwani kabla msanii huyo aondoke Nairobi kuelekea Mombasa wangekuwa wamekamilisha kila kitu mpaka kufikia asilimia 90.

“Uongozi wa Stevo Simple Boy unafaa kujiuzulu mara moja au nihakikishe wametiwa mbaroni. Mnaanzaje kumleta msanii kutoka Nairobi hadi Mombasa na hata hajalipwa senti moja. Kwani kazi yako kama meneja ni gani?” Omondi alitema moto kupitia Instastory yake.

Mchekeshaji huyo ambaye katika miezi ya hivi karibuni ameonekana kuwa mtetezi wa Sanaa ya muziki wa humu nchini alisema haelewi ni kwa nini msanii huyo wa Freshi Barida anakuwa na mameneja wane ambao wote wanashindwa kumshauri kimuziki kama inavyofaa.

Pia aliwatuhumu kwa kumchezea Stevo shere na kutumia gharama zake kubwa katika vyakula na kisha kumpandisha basi kurudi Nairobi.

“Halafu mimi nilikuja kutaarifiwa juu ya hili dakika ya mwisho nyuma ya ukumbi. Mnakula shilingi elfu 84 kwa vyakula na vinywaji wakati msanii wenu hajalipwa na mnampandisha basi kurudi Nairobi, lakini ni kwa nini Stevo ana mameneja 4?” Omondi alifoka.

Mchekeshaji huyo alisema yeye hakujua kama Stevo hajalipwa kwani alikuwa anajua kila mtu amelipwa pamoja na wacheza santuri wote lakini alipokuwa anamuita msanii huyo kupanda jukwaani ili kutumbuiza, ndio alitaarifiwa kuwa alikuwa bado anadai malimbikizi yake.

View Comments