In Summary

• Mchekeshaji huyo alikuwa akizungumzia umuhimu wa wanaume kuzungumza badala ya kujinyamazia.

Mchekeshaji Dr Ofweneke afichua kutaka kujitoa uhai.
Image: Instagram

Mchekeshaji Dr Ofweneke kwa mara ya kwanza amesimulia jinsi alijaribu kujitoa uhai kwa kujitia kitanzi mara tatu bila mafanikio.

Ofweneke ambaye alikuwa anazungumza katika podcast moja alibainisha kuwa kipindi hicho alikuwa mdogo, mwanafunzi wa darasa la tatu na fikira za kujitoa uhai zilimjia mara kwa mara, haswa baada ya wazazi wake kutengana wakiwa Nairobi na yeye alibaki kijijini na binamu yake.

“Wazazi wangu walikuja kugundua hili juzi tu, hakuna mtu alikuwa anajua kipindi chote hicho. Mimi nilijaribu kujitoa uhai mara tatu, lakini sikufanikiwa. Ya kwanza nilijaribu kufunga Kamba kwa nyumba, kwa sababu sikuwa naishi na wazazi wangu bali nilikuwa naishi na marehemu mjomba na shangazi yangu,” Ofweneke alihadithia.

Alisema kuwa alikuwa amejiwekea ratiba ya kutaka kujiua ambapo Jumatatu alikuwa anenda shule na siku inayofuata anaelekea msituni kutathmini njia ya kujitoa uhai.

“Kwa msituni nilikuwa nashinda huko siku mzima na kurudi usiku. Wakati huo wazazi wangu walikuwa Nairobi na walikuwa wametengana na nilikosa mtu wa kuangalia nikijiuliza mbona walikuwa wamenitupa hivyo. Nilikuwa darasa la 3 kipindi hicho.”

Mara ya kwanza alifunga Kamba kwa nyumba lakini kujaribu kujitia kitanzi, mbao ya nyumba ikakatika na akaanguka sakafuni, mara ya pili akaelekea msituni ili kupigwa na tumbili hadi afe.

“Tumbili walikuja wakaanza kunigwara na baadae watu wakakuja na kunisaidia lakini sikuwa nataka. Mara ya tatu nilijitupa mbele ya gari barabarani lakini lile gari likanikwepa na hivyo ndio nilifeli mbinu yangu ya tatu kujitoa uhai,” Ofweneke alielezea.

Ofweneke alisema kuna umuhimu wa wanaume kupewa ushauri wa kuweka wazimambo yanayowasumbua vichwani, tofauti na ilivyo kuwa wanaume wengi hawana nafasi kuonesha udhaifu wao.

Mcheshi huyo atakuwa mshereheshaji mkuu katika hafla ya kongamano la wanaume litakalofanyika mnamo Februari 14 katika ukumbi wa Carnivor jijini Nairobi.

Kongamano hilo litafanyika sambamba na siku ya Valentino na mwanahabari Stephen Letoo ambaye yuko mstari wa mbele kulipigia debe alisema moja ya masuala tete yatakayozungumziwa ni kuhusu afya ya akili ya mwanamume na umuhimu ya kufunguka kuhusu kinachokusibu.

View Comments