In Summary

• Mchungaji huyo aliwafokea wale wanaojiona kuwa wasomi wasioelewa Kiswahili na kuwataka wazime runinga zao.

• Ng'ang'a ambaye pia aiwahi kuwa jela alisema anatoa ushauri kwa watu wa jela jinsi ya kufanikiwa baada ya kifungo.

Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Image: Screengrab//Sasa TV

Mchungaji mwenye utata mwingi, James Ng’ang’a ameangusha mjeleedi mzito kwa wale ambao wanashinda kuikosoa lafudhi yake kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ambayo imeathirika pakubwa na lugha yake asili ya Kikuyu.

Katika video moja ambayo haijulikani ni yalini, Ng’ang’a anaonekana akitoa mzomo mkali kwa wale wanaomkosoa na kumrekebisha katika kutofautisha matamshi ya herufi L na R akisema kwamba mahubiri yake huwa hayawalengi wao.

Ng’ang’a alisema kuwa mahubiri yake ni mahususi kwa watu ambao hawakusoma, wale ambao walifungwa jela kama yeye na wale ambao riziki yao ni kutokana ka kuvuta mikooteni – makundi ya watu ambao haja yao kuu ni kupata neno na wala si kuzingatia jinsi maneno yanatamkwa.

“Usikae hapo ukinirekebisha hapo nimeweka R, hapo nimeweka L, zima runinga yako na ufungue ile runinga yenye matamshi yanafuatana vile ulifunzwa chuo kikuu. Lakini wale mko jela, wale tulikuwa jela nao, wale wa mkokoteni na wale maskini, mnisikilize. Mimi ndio nimetoboa, nimefika hapa nimefika naweza nikatoa ushauri kwenu jinsi ya kufaulu. Hata wale hamkusoma,” Ng’ang’a alisema.

Mchungaji huyo aliwafokea wale wanaojiona kuwa wasomi wasioelewa Kiswahili na kuwataka wazime runinga zao ili kufuata mahubiri kwa runinga za Kiiingereza.

“Wale hamjui Kiswahili mtajifundisha kama vile mimi najifunza kizungu. Na kama hautasikia Kiswahili tafuta mhubiri mwingine wa kizungu atakusaidia mwendelee. Si lazima wanyama wote wafanane, kuna punda na kuna farasi. Wale wa Kiingereza, zima runinga zenu na mfungulie runinga zenye mtapata ujumbe wa kuelewa,” Mchungaji huyo alisema.

Mchungaji huyo wa Neno Evangelism alisema kuwa ujumbe wake unawalenga wale wote wanaodharauliwa mradi tu wanajua kuhesabu moja hadi kumi pekee.

“Kama unajua kuhesabu tutapelekana, kama hujui, wewe rudi nyumbani. Mimi nakushauri njia ya kufanikiwa bora ujue kuhesabu. Nitakufundisha kuhesabu laki moja, ukifaulu nakupeleka hadi laki tano, hivyo hivyo,” alisema.

View Comments