In Summary

• “Tasnia ya injili inaonesha picha halisi ambayo mtu yeyote anapitia, kuna kupanda na kushuka." - Masika.

Mwimbaji wa Injili, Mercy Masika.
Image: Instagram

Msanii wa injili Mercy Masika amewataka Wakenya kukoma kuangazia yale mabaya katika mambo mbalimbali na kufumbia jicho yale machache mazuri.

 

Akizungumza kwenye kituo cha Radio Jambo na mtangazaji Masawe Japanni, Masika alisema kuwa ametembea kwenye mataifa mengi ya Afrika na amejionea jinsi watu wanaishi katika hali duni sana kuliko huku nchini.

Alisema kwa njia nyingi Wakenya wamebarikiwa lakini hawaoni, kisa kulalamika kwa kila kitu, huku pia akisema nguvu nyingi hutumika katika kuangazia masuala hasi katika jamii.

 

“Nimebahatika kutembea mataifa mengi ya Kiafrika na naweza sema Kenya tuna bahati sana, tumebarikiwa lakini hatuwezi jua mpaka pale tutakapofika kule nje. Unaenda nchi zingine unakuta watu wanatembea wakiwa wamejihami kwa bunduki hadi unaingiwa na mchecheto. Wakenya tuache kulalamika kwa kila kitu. Vyombo vya habari vingi huwa wanachukua mambo ya hasi tu na kuwekeza muda mwingi huko,” Masika alisema.

 

Msanii huyo aliyetamba kwa kibao ‘Mwema’ alifutilia mbali madai kwamba tasnia ya muziki wa injili nchini inaelekea kufifia na kusema kwamba huu ndio muda kuna ukombozi mkubwa kwenye injili kuliko muda mwingine wowote.

 

“Tasnia ya injili inaonesha picha halisi ambayo mtu yeyote anapitia, kuna kupanda na kushuka. Inawezekana ndio kuna kulegea mahali lakini hilo halimaanishi kwamba injili inafifia, nahisi kuna ukombozi mkubwa wakati huu kuliko wakati mwingine wowote,” alisema.

Kama Solomon Mkubwa, Masika pia alikubaliana kwa kiasi Fulani katika matamshi ya Eric Omondi kuhusu kashifa kuu aliyoitoa kwa wasanii wa injili na kusema kwamba anahisi mchekeshaji huyo angezungumza kwa njia ya mapenzi Zaidi kuhusu baadhi ya wasanii aliowataja kwenye video yake.

 

View Comments