In Summary

• Mwaka jana, Diamond Platnumz aliwakilisha ukanda wa Afrika Masahriki tamasha hilo lilipofanyika nchini Ureno.

Sauti Sol kuchukua nafasi ya Diamond Platnumz Afronation.
Image: Instagram

Afro Nation, waandaaji wa tamasha kubwa Zaidi duniani la miziki ya Afrobeats wametoa orodha ya wasanii ambao watatumbuiza kwenye sherehe za mwaka huu.

 Katika orodha hiyo, imetawaliwa na wasanii wengi kutoka mataifa ya Afrika Magharibi haswa Nigeria ambako ni chimbuko la miziki ya Afrobeats, huku kwa mara ya kwanza bendi ya Sauti Sol ikiorodheshwa na kuwa wawakilishi wa pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Miamba kama Davido, Burna Boy, Ayra Starr, Oxlade, Wizkid, Asake, Black Sheriff, Fireboy DML, na bendi ya muda mrefu kutoka Kenya Sauti Sol ni miongoni mwa watumbuizaji walioorodheshwa kwenye bango rasmi.

Kikubwa kilichozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii haswa ukanda wa Afrika Mashariki ni kukosekana kwa jina la msanii hata mmoja kutoka Tanzania, licha ya wasanii wengi kujitutumua kwa hali na mali muda mrefu kuibeba ramani ya ukanda huo kwenye mabega yao kimuziki.

Ila Watanzania msikonde, Sauti Sol kutoka Kenya safari hii wataipeperusha bendera ya jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo mwaka jana msanii Diamond aliipeperusha tena vizuri tu.

Mwaka jana tamasha hilo lilipokuwa likifanyika nchini Ureno, msanii Diamond Platnumz alikuwa mmoja na wa pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki ambaye aliwakilisha na kutumbuiza baina ya mibabe wa miziki ya Afrobeats.

Kipindi hicho, Platnumz alikuwa katika ziara ya Ulaya kuitambulisha nusu albamu yake ya FOA.

Kukosekana kwa Diamond kumevutia hisia mbalimbali mitandaoni, baadhi wakihisi mwaka huu hajafanya vizuri katika miziki ya kusikilizwa kimataifa, licha yay eye kutangaza kuwa ndio mwaka wa nunda juu ya nunda kuachia miziki mchanganyiko.

Msanii huyo alianza mwaka kwa vishindo vya aina yake kwa kuachia miziki kadhaa ambayo hata hivyo licha ya kutajwa kuwa tungo nzuri, ilisemekana kuwa ya kuwavutia tu watu wa Afrika Mashariki ambao wanakipungia pakubwa Kiswahili.

 

View Comments