In Summary

• “Namfuata sana Jay Z kwa nia ya kujifunza kwa sababu tuko sehemu moja. Sisi sote ni waburudishaji." - Nadia Mukami,.

Nadia afuata nyayo za Jay Z
Image: Instagram, Forbes

Mwanamuziki Nadia Mukami amefunguka kwamba nia na uchu wake wa kutafuta utajiri usiku na mchana ni kutokana na msukumo ambao anaupata kutoka mwanamuziki mkongwe wa Marekani, Jay Z.

Katika mahojiano ya kipekee na Sunday Nation, Mukami alisema kwamba tangu utotoni amekuwa akimfuatilia kwa ukaribu Jay Z jinsi alijiweka katika kupata mapato kwa njia mbali mbali kando na muziki.

“Namfuata sana Jay Z kwa nia ya kujifunza kwa sababu tuko sehemu moja. Sisi sote ni waburudishaji. Namaanisha, kama ulijali kusikiliza mazungumzo yake kwenye kipindi cha gumzo cha Kevin Hart ‘Hart to Heart’, Jay Z anazungumzia umuhimu wa kuwa na njia nyingi za mapato,” Mukami aliambia jarida hilo.

Mukami alisema kwamba wasanii wengi wa Kenya hupata pesa nyingi sana kutoka kwa mitikasi ya Sanaa, wakati mwingine hata Zaidi ya milioni moja kwa mwezi.

Alisema kwamba wasanii wengi hutumia pesa hizo vibaya wakiwa na dhana maishani kwamba pesa nyingi zitaendelea kuja, jambo ambalo alilitaja kuwa kutahadharisha maisha.

“Maisha hutokea. Mambo yanaweza kwenda vibaya sana. Nani angewahi kufikiria janga la Covid-19?" Mukami aliuliza.

Mpaka sasa, Mukami amefungua biashara mbali mbali ikiwemo studio ya muziki na saluni ambayo alisema kwamba ana wafanyikazi 25 ambao anawalipa.

Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Maseno ni mtaalamu wa fedha kwa mafunzo, mburudishaji kwa mazoezi, mfadhili, mfanyabiashara na mama, shughuli anazocheza kwa urahisi licha ya shinikizo la maisha.

Alisema kwamba anataka kujitahidi mpaka kuona lebo yake ya muziki ya Sevens Creative ikiorodheshwa kwenye soko la hisa la Nairobi.

"Nimejifunza sio tu kutegemea muziki. Ndani ya nchi, ninawatazamia watu kama Peter Nduati, ambaye alijipatia pesa kutokana na sekta ya bima na muziki kupitia lebo yake ya Pine Creek Records. Watu wengi katika tasnia ya muziki hawajui hata kuwa unaweza kupata pesa kwa kumiliki nakala kuu za wasanii chini ya lebo yako ya rekodi. Mwingine ni Myke Rabar, Mkurugenzi Mtendaji wa Homeboyz Entertainment. Ni kampuni ya kwanza na ya pekee ya burudani iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi. Sevens Creative Hub (kampuni yake) hakika itakuwa ya pili," Nadia anasema.

View Comments