In Summary

•Omondi alisema iwapo Azimio hawataweka maandamano kila siku, yeye atweka yake siku ya Jumatano na Ijumaa.

Msanii Eric Omondi amemwomba kinara wa Azimio Raila Odinga kuweka maandamano kila siku.

Eric amedai kuwa maandamano ya kila siku ili kukwamisha shughuli zote nchini. 

Omondi alimsuta naibu rais Rigathi Gachagua kwa kusema kuwa wawekezaji na wafanyibiashara walipoteza pesa nyingi kutokana na maandamano na ilhali yeye, rais William Ruto na mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi walijitengea shilingi milioni 802 kununua magari mapya.

"Ningependa kumwomba mheshimiwa Raila Odinga kufanya maandamano kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumatatu...Gachagua alisema kuwa serikali inapoteza ila walipewa shilingi 802 milioni kununua magari," alisema Omondi.

Omondi alisema maandamano yatafanya serikali pia kupoteze pesa kama hali ilivyo kwa wananchi wa kawaida. Aliongezea kuwa wako tayari kujiunga na maandamano hayo.

Eric alidai kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanahangaika ilhali wachache ndio wanapata raha hivyo basi ni bora kila mtu awe sawa kwa kuhangaika.

Alisema haya huku akitoa mfano wa vijana aliowalipia faini ili waachiliwe kutoka korokoroni kwa kukosa shilingi mia tano.

Alipoulizwa kuhusu viongozi kufanya mazungumzo, msanii huyo mwenye miaka 41 alidai kuwa kuongea kutafanywa wakati serikali itashusha gharama ya maisha ili watu wasiumie zaidi.

Eric Omondi amekuwa akiandaa maandamano katika majengo ya bunge dhidi ya gharama ya juu ya maisha. Mara ya mwisho alishikwa na polisi na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu 150,000.

Kinara wa muungano wa Azimio, Raila Odinga, ameitisha kufanyika kwa maandamano ya amani siku za Jumatatu na Alhamisi, kila wiki.

 

View Comments