In Summary

• “Hongera @djfatxo kwa kushinda msanii wa kiume mugithi wa mwaka africa mashariki katika Tuzo za E360 toleo la nne 2022/23. AMINI, saga, KUWA,” E360 waliandika.

DJ Fatxo ashinda tuzo ya Msanii bora.
Image: Instagram

Mcheza santuri na msanii wa miziki ya Agikuyu almaarufu Mugithi, DJ Fatxo amejishindia tuzo ya kifahari ya e360 Jumanne, huku jina lake likizidi kuwa moja ya majina yaliyotajwa sana mitandaoni kwa kashifa ya kifo cha utata cha aliyekuwa rafiki yake, mbunifu wa mitindo, Jeff Mwathi.

Msanii huyo alidokeza kwa mashabiki wake mwezi jana kuwa ameteuliwa kuwania tuzo hizo katika kitengo cha msanii bora wa nyimbo za Mugithi kitengo cha wanaume. Aliwarai wafuasi wake kumpigia kura kwa wingi kipindi hicho kabla ya kashifa hiyo kutanda.

Tuzo za e360 hufanyika nqa kuwajumuisha wasanii katika ukanda wa mataifa ya Afrika Mashariki ambazo dhima yake ni kuwatambua na kuwatuza wasanii wa ukanda huu kwa kazi zao nzuri kwenye Sanaa.

“Hongera @djfatxo kwa kushinda msanii wa kiume mugithi wa mwaka africa mashariki katika Tuzo za E360 toleo la nne 2022/23. AMINI, saga, KUWA,” E360 waliandika Instagram baada ya kumkabidhi msanii huyo tuzo hiyo.

Washindi wengine ni pamoja na Meshack Mwengei aliyekuwa msanii wa kiume aliyepigiwa kura nyingi zaidi, Phelix Owiny (Mwanamitindo Bora wa Kiume wa Mwaka), Joseph Sonko Jnr (Mwenye uwezo tofauti wa Mwaka), Fred Muyanga (Msanii Bora wa Mwaka wa Injili) na Sarafina Salim (Msanii wa Kike Mugithi. ya mwaka).

Kwa takribani mwezi mmoja sasa, msanii huyo amejipata katika hali ngumu ya kujieleza baada ya makundi mbalimbali mitandaoni kumhusisha na kifo cha utata cha rafiki yake Jeff Mwathi. Mwathi alisemekana kufariki katika nyumba ya msanii huyo mtaa wa Kasarani jijini Nairobi katika hali ya ukakasi, Fatxo na wengine waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wakiandikisha ripoti kuwa alijitupa kutoka ghorofa ya kumi.

Hata hivyo, baada ya mazishi kukamilika, wanaharakati walihisi kulikuwa na utata mwingi uliozingira kifo cha kijana huyo na kutoa ombi kwa idara ya upelelezi DCI kufanya uchunguzi wa kina, wakihisi kwamba huenda kijana huyo ni mwathirika wa ulawiti.

DCI walivalia njuga suala hilo na awamu ya kwanza ya uchunguzi huo ilibaini kwamba Mwathi aliuawa wala hakujiua kama ilivyosemekana hapo awali.

Awamu ya pili ya uchunguzi huo inaendelea na mwili wa Mwathi unatarajiwa kufukuliwa Ijumaa wiki hii kama njia moja ya kubaini ukweli wa kilichosababisha kifo chake nyumbani kwa Fatxo.

View Comments