In Summary

• "Watu wa boda boda wako Jela na mama mboga amefungiwa Pumwani,” Omondi alitoa wito.

• Omondi anafanya kitendo hicho siku chache baada ya kusaidia kulipa dhamana ya mwanabodaboda aliyelia kortini.

Eric Omondi awatoa kina mama waliokuwa wamezuiliwa hoospitali ya Pumwani.
Image: Instagram

Kwa mara nyingine tena mchekeshaji Eric Omondi ameendeleza na huduma yake ya kutoa msaada kwa wasiojiweza katika jamii baada ya kuwalipia mama waliokuwa wameshikiliwa katika hospitali ya kujifungua mama wajawazito ya Pumwani.

Kupitia Instagram yake, Omondi alidokeza kwamba aliwalipia kina mama watano ambao baada ya kujifungua, walikosa hela za huduma na ikabidi washikiliwe na watoto wao wachanga hadi pale watakapolipa bili hiyo.

Omondi ambaye hivi karibuni amedokeza kuacha ucheshi na kuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu alitoa wito kwa rais Ruto kabla ya kuwateua wasaidizi wa mawaziri 50 na kuwanunulia magari ya kifahari, atoe agizo kwa hospitali zote nchini ikiwemo Pumwai ambapo kina mama wanashikiliwa na watoto wachanga kuachiliwa.

“Tumewaachilia kina mama Wapya 5 waliokuwa wamezuiliwa katika Uzazi wa Pumwani. Mheshimiwa Rais kabla hujalipa mabilioni ya pesa kwa CAS 50, kabla ya Serikali kununua magari mapya kabisa kwa ajili yao, TAFADHALI toa agizo kwa Akina Mama wote waliozuiliwa Pumwani na Nchi nzima waachiwe. Ulisema Serikali ni ya Mama mboga na Boda Boda. Watu wa boda boda wako Jela na mama mboga amefungiwa Pumwani,” Omondi alitoa wito.

Kitendo hiki kinajiri siku chache tu baada ya Omondi kulipa dhamana ya shilingi elfu 25 kwa ajili ya mwendesha bodaboda ambaye alifikishwa mahakamani na kutakiwa kulipa dhamana hiyo ili kuachiliwa.

Mhudumu huyo wa boda alijitupa chini kwa mfadhaiko na kuaga kujigaragaza akilia kwamba hangeweza kumudu kiasi hicho cha dhamana.

Omondi pia wiki kadhaa zilizopita alimtoa mwanadada mmoja aliyekuwa amefungwa jela ya wanawake ya Lang’ata kwa kukosa faini ya shilingi elfu 10 baada ya kukamatwa na ‘kanju’ jijini Nairobi akipiga kelele kuita wateja kwa ajili ya biashara aliyokuwa ameajiriwa.

View Comments