In Summary

• "Daima tendea wengine mema yatakurudia kwa njia usiyotarajia na kuomba ulinzi maana kuna mengi hatuyaoni.” - Fatxo.

DJ Fatxo asherehekea kufikisha miaka 27
Image: Instagram

Mcheza santuri na mwimbaji wa nyimbo za Mugithi, DJ Fatxo Jumanne alisherehekea kufikisha umri wa miaka 27, huku sakata la kumhusisha na kifo cha mbunifu Jeff Mwathi likionekana kufifia.

Fatxo alinukuu Kifungu cha Biblia akisema kwamba alikuwa mdogo na sasa ni mkubwa lakini hajawahi ona mtoto wa maskini akikosa mkate wala kuomba chakula na kumtaka Mungu kumzidishia ili asiwahi kosa.

"Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, lakini sijamwona mwenye haki ameachwa, Wala wazao wake wakiomba chakula." ~ Zaburi 37:5” Fatxo aliandika.

Msanii huyo ambaye amepitia wakati mgumu kwa kuhusishwa na kifo cha Mwathi kwa Zaidi ya miezi miwili sasa alisema kuwa haujakuwa muda rahisi kwake akiwa na miaka 27 na kutaka mwaka wake wa 27 maishani kuwa mzuri kwani yuko tayari kupitia magumu kama dhahabu ipitayo kwa tanuru la moto kabla ya kuwa madini yenye thamani kubwa.

“Nina furaha kusherehekea mwaka mwingine wa maisha yangu. Furaha ya Kuzaliwa kwangu! Asante sana, Mungu kwa kunipa mwaka mwingine wa maisha. 27 tafadhali kuwa mkarimu mwaka huu uliopita utakuwa wa kutafakari kila wakati... nimepitia mengi kama Dhahabu ambayo lazima ipitie kwenye tanuru lakini ukweli wa ajabu zaidi ni kwamba, sizeeki, ninazidi kuwa mzoefu,” Fatxo alisema.

Mcheza santuri huyo alijihongera kwa kuwa mkakamavu wakati ambapo ilionekana kila mmoja hakutaka kujihusisha naye haswa haswa kufuatia kifo cha utata cha rafiki yake Mwathi ambaye baadhi walihisi kwamba alilawitiwa kabla ya ‘kutupwa’ kutoka ghorofani.

“Ninashukuru kwa kustahimili changamoto zote katika siku 365 zilizopita na kutimiza mwaka mmoja zaidi. Daima tendea wengine mema yatakurudia kwa njia usiyotarajia na kuomba ulinzi maana kuna mengi hatuyaoni.”

Mapema wiki jana, DCI walisema kuwa uchunguzi wa pili dhidi ya kifo cha Mwathi ulikuwa umekamilika na faili ya kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa kwa DPP kutathmini iwapo mashtaka yatafunguliwa au la.

 Hata hivyo, za ndani zilidai kwamba DCI walipata uchunguzi huo hakuna vile umemhusisha Fatxo na kifo cha Mwathi, kinyume na ripoti ya awamu ya kwanza ya uchunguzi iliyosema Mwathi aliuawa.

View Comments