In Summary

• Tuligundua kuwa baadhi ya nyuki walikuwa wamevamia mzinga ambao ulikuwa umetegwa kichwa chini - Charlene.

Charlene Ruto afichua sababu ya kuita mzinga Bottom Up.
Image: Twitter

Binti wa kwanza wa taifa Charlene Ruto kando na kufuata nyayo za babake katika siasa, pia ni mwanafunzi mzuri katika suala la ukulima kutoka kwa wazazi wake.

Charlene Ruto wikendi iliyopita alifichua kwamba ni mkulima mahiri wa ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kurina asali ya biashara.

Charlene alipakia rundo la picha na video akiwa kwenye shamba lao la nyuki huko Eldoret kaunti ya Uasin Gishi ambapo alikuwa amevalia mawanda kamili ya warina asali ili kujikinga kutoka mishale ya nyuki.

“Nilikosa nyuki wangu na nikaamua kurudi nyumbani Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu na nikaamua kuzuru shamba wikendi iliyopita,” Binti wa kwanza wa taifa alisema.

Hata hivyo, kilichowakosha wengi ni kuona mzinga mmoja uliokuwa umeandikwa “Bottom Up” kauli maalum ambapo babake aliitumia sana katika manifesto yake wakati wa kampeni za urais mwaka jana.

Charlene hata hivyo hakusita kutoa sababu ya kuuita mzinga huo kwa jina hilo.

“Tulipokuwa tukifanya ukaguzi kwenye mizinga, tuligundua kuwa baadhi ya nyuki walikuwa wamevamia mzinga ambao ulikuwa umetegwa kichwa chini na kuanza kutengeneza masega ya asali. Tuligeuza mzinga kuwa wima, tukavuna asali iliyopo na kuupa jina la "Bottom Up" kwa uchunguzi rahisi wa maendeleo yake,” Charlene alifafanua.

Binti wa rais alitumia fursa hiyo kuwashauri wananchi kwamba suala la ufugaji wa nyuki ni jambo la kijamii na kila mtu anaweza kulikumbatia ili kujiendeleza.

“Ufugaji wa nyuki ni shughuli ya jumuiya kwa sababu tunasaidiana katika kuwezesha hali bora za nyuki, kuuza asali yetu na kukuza kila mmoja katika ujuzi wetu,” alisema.

View Comments