In Summary

• Kulingana na yeye, kila msanii anapaswa kujitahidi kuwa bora katika kile anachofanya na kuuchukulia muziki kama biashara zao.

Jaguar afichua sababu ya wasanii wa Kenya kuishi maskini
Image: Instagram

Siku kadhaa baada ya kuongoza mchakato wa kumchangia msanii mwenzake Colonel Mustafa, Jaguar ametoa maoni yake kuhusu ni kwa nini wasanii wengi wa Kenya wanatatizika katika muziki na kifedha.

Akizungumza wakati wa mahojiano ya hivi majuzi kwenye redio, mwimbaji wa ‘Kigeugeu’ alianza kwa kueleza kuwa wasanii wengi hawachukulii ufundi wao kwa uzito jinsi wanavyopaswa.

Kulingana na yeye, kila msanii anapaswa kujitahidi kuwa bora katika kile anachofanya na kuuchukulia muziki kama biashara zao.

“Ninachotaka kuwaambia wasanii leo kwa sababu mimi binafsi nimejitahidi kabla sijatoa Kigeugeu. Nilikuwa nimejitahidi kwa miaka kama 10. Shida ya wasanii wetu ni kwamba hawachukui muziki kama biashara,” mbunge huyo wa zamani wa Starehe alisema.

Kulingana na Jaguar, talanta ya Wakenya inachohitaji ni ushauri utakaowasaidia kutambua uwezo wao kamili. Kwa maneno yake, kila msanii anayetoa muziki katika siku hizi na zama hizi anapaswa sit u kuangalia ushindani wa humu nchini bali pia ushindani wa wasanii wa kutoka nje ya Kenya na ambao nyimbo zao zinafanya vizuri ndani na nje ya nchi.

Mbali na kufanya muziki wa wastani, mwanasiasa huyo aliendelea kueleza kuwa wengi wao hawahifadhi mapato wanayopata kutokana na muziki wao na hivyo kuishia kuharibika na kukosa matumaini nyakati zinapokuwa ngumu.

“Nasikia baadhi ya watu wakisema muziki hauna pesa na ni kwa sababu hawana akiba. Ni kweli kwa sababu kwangu nilichokifanya nilipoingia kwenye biashara ya muziki nilijua hakuna biashara ambayo haina tabu. Kwa hivyo ikiwa hutahifadhi au kufikiria kuhusu mawazo mapya utafunga biashara hiyo, "aliongeza.

Kwa maoni ya Jaguar, kusaidia wasanii kumeendelea kuwa changamoto kwani hawapatikani kila mara kwa ajili ya kukaa chini ili kujadili mambo yanayowahusu hata wakati jukwaa linatolewa.

Pia alizungumzia mswada wa mcheshi Eric Omondi ambaye anataka miziki ya wasanii wa Kenya kupatiwa kipaumbele cha hadi asilimia 75 kwenye media zote, lakini akasema hilo pekee haliwezi kuwasaidia wasanii.

"Kwa hivyo nataka tu kuwaambia wasanii kwamba shida zao hazitaisha bungeni. Eric anaendelea kuzungumza juu ya 75%. 75% hawatatoka bungeni kwa sababu ni juu yetu kufanya muziki mzuri,” alimalizia.

View Comments