In Summary

• Zari katika picha za hivi karibuni ambazo amezichapisha kwenye Instagram yake, zikiwemo video, Shakib hakuonekana naye kama ambavyo imekuwa kawaida yao.

Shakib ajitia moyo baada ya msukosuko kukumba penzi lake na Zari.
Image: Instagram

Mume wa mfanyibiashara maarufu wa Uganda mwenye makao yake nchini Afrika Kusini, Zari Hassan, Shakib Cham Lutaaya amejiliwaza na maneno ya kiume, akidokeza kwamba yeye hajapoteza kitu chochote licha ya msukosuko baina yake ya Zari.

Ikumbukwe siku chache zilizopita mitandao ya kijamii iliwaka moto baada ya promota wa Zari anayeishi nchini Uingereza kuvujisha sauti jinsi walivyokuwa wanazungumza na mfanyibiashara huyo kuelekea shoo yake ya huko Birmingham.

Katika sauti hizo, Zari alisikika akitoa maelekezo kwa promota huyo jinsi ya kumpokea mumewe Shakib ambaye kwa mujibu wake angesimama upande wake kama meneja wake.

Lakini kile ambacho kiliwaacha wengi katika gumzo ni kwamba Zari alimuelezea mumewe kama fala na mtu ambaye hajiamini mbele za watu, na hivyo kumtaka promota huyo kutomchukua mbio wakati atasimama kama meneja wake.

Tamko hilo la kumuita Shakib kama fala liliwaacha wengi katika hali ya utashi, huku hadi Shakib mweneywe akionekana kughadhabishwa na kuhisi kukatishwa tamaa na mwanamke ambaye alimpenda mpaka kufunga ndoa ya kiislamu na yeye mwezi Aprili.

Shakib hata hivyo amesimama na kujikung’uta mavumbi na kujitia moyo kwa maneno ya kiume akisema kuwa bado yeye ni bingwa wa maisha wala hajapoteza chochote.

“Bingwa wa maisha,” Shakib aliandika kwenye picha yenye kutamauka aliyoipakia kwenye Instagram yake.

Juzi Shakib alitupa dongo kwenye domo la Zari alimtuhumu kwa kumvua nguo mbele ya hadhira, huku akiashiria kwamba mwanamke huyo ambaye anamzidi umri mara dufu huenda ana kiburi na ambacho kitamgharimu pakubwa ikiwemo kumpoteza.

Zari katika picha za hivi karibuni ambazo amezichapisha kwenye Instagram yake, zikiwemo video, Shakib hakuonekana naye kama ambavyo imekuwa kawaida yao tangu kufunga ndoa miezi miwili iliyopita.

Baadhi ya mashabiki wao wanahisi kuna jambo linatokota baina ya wanandoa hao wapya na halitokaa kitambo kirefu kabla ya kulipuka.

Ila kwa sasa wote tumeketi mkao wa kula tukisubiria, nini baadae!

View Comments