In Summary

• Owen aliwakosoa wale ambao walihisi kuvunjika moyo kwa kutoona picha ya mwanawe.

• Msanii huyo wa injili alisema hakuwa na nia ya kuchapisha ujumbe kwa ajili ya watu bali kwa ajili ya kumsherehekea mwanawe.

Daddy Owen Kwa nini sikutumia picha ya mwanangu kumtakia heri njema ya siku ya kuzaliwa.
Image: Facebook

Jumatano jioni, msanii wa injili ambaye pia ni mwanaharakati wa kutetea haki za watoto wenye ulemavu Daddy Owen alimsherehekea mvulana wake kutimiza mwaka mwigine.

Lakini kilichowashangaza wengi ni kwamba msanii huyo hakupakia picha ya mtoto wake, kama ambavyo wengi walitarajia, badala yake alipakia picha ya simba na kuandika ujumbe mtamu kwa mwanawe.

Baadae mwandishi wa Radio Jambo alifanya mazungumzo ya kipekee na msanii huyo kwa njia ya simu tukilenga kujua kwa nini hana uraibu wa kupakia picha za wanawe kwenye mitandao ya kijamii.

Owen alisema kuwa asingependa kuwa yule mzazi ambaye anamchagulia mtoto maisha yake na kumsababishia presha zisizostahiki kwa kumtambulisha mitandaoni.

“Mimi muda wote huwa nasema, mwisho wa siku mwenyewe nilichagua nilichotaka kuwa, unanielewa. Nilichagua kuwa msanii, kuwa mwinjilisti. Hakuna mtu alinilazimisha kuwa mtu maarufu, na hakuna mtu alinilazimisha. Kwa hiyo hata kwa watoto wangu huwa nasema ikiwa mbeleni watataka kuwa wasanii ni chaguo lao. Sidhani kama ni vyema kuwachagulia sasa hivi,” Owen alitetea hatua yake ya kutopakia mwanawe mitandaoni.

Msanii huyo alisema kuwa kwa vile yeye ni maarufu, kuwatambulisha wanawe mitandaoni kutakuwa kama njia moja ya kuwawekea shinikizo la kutambuliwa kila mahali na kupitia kila kitu wafanyacho kuwa ni ‘watoto wa Daddy Owen’.

“Wakati unaweka presha kwao [watoto] hata masomo yao shuleni, watakuwa wanamulikwa, huyu ni mtoto wa nanii, anakuwa namba 4, namba 10… sitaki kuwaweka watoto wangu kwa hiyo presha,” aliongeza.

Kwa kurejelea chapisho lake, Owen alikuwa makini pakubwa kutolitaja jina la mtoto huyo wala kusema alikuwa anafikisha miaka mingapi. Kwa nini?

“Wakati mwingine mimi husema vitu vingine kama hivyo wacha tu abaki navyo. Mimi najua tu nimemsherehekea nimesikia poa nini… ili pia huko mbeleni asije kujihisi vibaya kwamba babangu hakunisherehekea. Atajua nampenda,” alisema Owen.

Owen aliwakosoa wale ambao walihisi kuvunjika moyo kwa kutoona picha ya mwanawe akisema kuwa yeye alichapisha ujumbe wa kumtakia mwanawe kheri ya kuzaliwa, wala hakuwa na nia ya kuchapisha kwa sababu ya watu.

View Comments