In Summary

• Eric alibainisha kuwa wazo la kumhamisha Stevo Simple Boy kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera hadi eneo lingine lilikuwa wazo lake kwanza.

• Omondi aliongeza kuwa hela hizo ambazo alikuwa amsaidie Stevo nazo sasa atazitumia katika mpango wake wa kuwasaidia watu wanaohangaika nchini.

Mchekeshaji Eric Omondi adai Mbunge wa Mumias East aliichukua wazo lake la kumsaidia Stevo Simple Boy.

Mchekeshaji aligeuka na kuwa mwanaharakati wa haki za kibinadamu na mkosoaji mkuu wa utawala wa rais Ruto, Eric Omondi amemkashifu Mbunge wa Mumias East, Peter Salasya kwa kile alichokitaja ni kuiba wazo lake la kumsaidia mwanamuziki Stevo Simple Boy.

Eric akizungumza kwa njia ya kipekee na mwandishi wa Radio Jambo, Moses Sagwe. alibainisha kuwa wazo la kumhamisha Stevo Simple Boy kutoka mtaa wa mabanda wa Kibera hadi eneo lingine lilikuwa wazo lake kwanza.

"Sasa nilisema nitasaidia Stevo Simple Boy, na baada ya siku tatu nikaona mbunge Fulani alienda na kufanya kila kitu nlikuwa nimesema nitafanya. Nilikuwa nimesema nitamlipia kodi ya miezi minane na shopping ya 5 months. Huyo mheshimiwa akaenda akafanya kila kitu exactly vile nlikuwa nimesema."

Rais huyo wa uchekeshaji Afrika, alisema alishangazwa siku moja baada ya kuamka na kupata mbunge huyo akiwa tayari ashamzawadi mwanamuziki huyo ambaye amekumbwa na matatizo ya kifedha.

Omondi aliongeza kuwa hela hizo ambazo alikuwa amsaidie Stevo nazo sasa atazitumia katika mpango wake wa kuwasaidia watu wanaohangaika nchini.

“Hio pesa wacha sasa niendelee kupea watu unga. Lakini kitu mzuri hapo ni kuwa either way Stevo alisaidika na hiyo ndiyo furaha yetu kama wasanii.”

Mapema mwezi huu, Mbunge huyo alitimiza ahadi yake kwa mwimbaji Stevo Simple Boy ya kumpatia makazi ya heshima.

Mwanasiasa huyo kijana aliwapeleka Stevo na mke wake Grace Atieno hadi kwenye nyumba aliyowatafutia jijini Nairobi na kuthibitisha kwamba tayari alikuwa amemaliza kuilipia kodi.

Mbunge huyo anayehuduma muhula wake wa kwanza katika bunge la kitaifa alithibitisha kuwa atamrudisha mke wa Stevo, Grace Atieno shuleni kwa kozi fupi ya masuala ya urembo ili awe na ujuzi utakaomsaidia kukidhi mahitaji yake na kusaidia familia yao ndogo.

“Nitamlipia shule ili aweze kujikimu. Pia nitamfungulia duka la nguo ili aweze kujisimamia ili bwana akienda shoo akipata ama asipopata kwa nyumba bibi atakuwa sawa. Wawe wanasaidiana,” Salasya alisema.

Aidha, Salasya aliendeleza ahadi zake kwa mwanamuziki huyo akisema iwapo atafikiria kujitosa katika kazi zingine za kutengeneza pesa mbali na muziki alikuwa tayari kumsaidia kwa njia yoyote.

"Pia nilisema wale ambao waliahidi kumjengea kama hawatafanya hivyo ndani ya siku 15 zijazo nitaenda Oyugis nimtengezee nyumba huko alafu aanze hapo," alisema mbunge huyo.

View Comments