In Summary

• KRG kama mfanyibiashara alisema kuwa huwa anaathirika pakubwa kila siku maandamano yanapofanyika.

• "Mimi kwa siku moja ninapoteza Zaidi ya milioni kama 5 au 6. Niko na biashara nyingi sana,” alisema.

KRG atoa tamko lake kuhusu maandamano.
Image: Screengrab

Msanii anayejiita tajiri wa kiwango cha bilionea nchini KRG the Don ametoa ujumbe wa kuchekesha kwa wale wanaojitokeza barabarani na mitaani kushiriki katika maandamano ya Azimio ambayo yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu.

Katika mahojiano na SPM Buzz, KRG aliwataka watu hao wanaoshiriki maandamano kisa ni kupanda kwa gharama ya maisha na mfumko wa bidhaa muhimu kuacha kufanya vitendo hivyo.

KRG alisema kuwa wengi wanaandamana kwa kisingizio cha kupanda kwa bei ya unga wa ugali, akiwaambia kwamba si lazima mtu ale ugali na badala ya kuandamana ni heri wale vyakula vingine na waache kusumbua wengine wasiotaka kuandamana.

“Unga umepanda, feelings, si mtafute ile poshomill bei rahisi ukae hapo. Kama unaona unga umepanda, kula chips, acha kusumbuka dunia hii. Ama tafuta kitu kingine, vyakula ni vingi. Ongeza akili. Duniani ukitumia sana feelings utaumia sana roho,” alisema.

KRG alisema kuwa hata kwa dawa yeye hawezi kushiriki maandamano kwa kile alisema kuwa huleta uharibifu wa mali.

“Mimi kama msanii nitakuwa nimesimama mahali ninaangalia tu kwa sababu mimi sitaki maandamano kwa sababu inaleta uharibifu wa mali, biashara za watu pia hazitafunguliwa, kuna watu wengine pia watalala njaa….ni watu wangapi unafikiri watalala njaa? Mimi nasema ni heri nifanye kazi ili nile kuliko kulala njaa kisa sikuhangaika. Kama maisha yamepanda tuongeze akili, tutafute pesa nyingi,” KRG alisema.

KRG kama mfanyibiashara alisema kuwa huwa anaathirika pakubwa kila siku maandamano yanapofanyika akisema kuwa huwa anapoteza pakubwa kwa kufunga biashara zake nyingi.

“Napoteza pesa nyingi sana kwa sababu kila siku ya maandamano inamaanisha nafunga biashara zetu zote. Kila kitu kinarudi chini. Sioni kama maandamano inaturudisha chini. Mimi kwa siku moja ninapoteza Zaidi ya milioni kama 5 au 6. Niko na biashara nyingi sana,” alisema.

KRG alikuwa na ujumbe huu kwa wananchi;

“Kama wewe unataka kwenda kuandamana kuchoma biashara za watu au kupiga mtoto wa watu mawe, naomba Mungu akubariki na wewe upate halafu siku nyingine mandamano yafanyike na wewe ufanyiwe hivyo usikue vile inauma.”

View Comments