In Summary

• Bahati amewataka wanamuziki wa humu nchini kuimarisha kazi yao ili kuweza kushindana na wenzao kutoka Tanzania.

• Bahati aliwahimiza wasanii hao kushirikiana ili kuweza kuvuka mipaka ya Kenya na kueneza muziki wa Kenya kote duniani.

Bahati
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Kelvin Bahati amejitokeza kimasomaso na kuwataka wasanii Wakenya kuamka na kuimarisha kazi yao ili kupigania nafasi yao katika muziki wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Mpenzi huyo wa Diana Bahati, katika taarifa yake ya Jumapili jioni alifafanua kuwa muziki kutoka kwa majirani wetu Watanzania umeendelea kutupiku kwa kiwango kikubwa kwa muda sasa.

“Wasanii wenzangu wa Kenya, tunaweza jaribu kupuuza hili lakini ukweli ni kuwa tumeacha jirani analala hadi na bibi zetu. Kuanzia Youtube, Boomplay, Itunes hadi kwa redio na runinga zetu.” ilisoma ujumbe huo wa Bahati.

Baba huyo wa watoto wanne, alieleza masikitiko yake baada ya kufika katika mtandao wa YouTube na kupata nyimbo za wasanii kutoka nchi ya Tanzania zikiongoza orodha ya nyimbo zinazovuma sana nchini Kenya, kuanzia nambari ya kwanza hadi nambari ya 10.

Katika kauli yake, Bahati aliwataka wanamuziki wote wa nchini kushirikiana pamoja akisema kuwa hakuna mwanamuziki anayeweza kueneza muziki wake nje ya mipaka ya Kenya binafsi ila ni kwa ushirikiano na wanamuziki wengine.

“Huu ndio muda mwafaka kwa wanamuziki wa Kenya kuacha kufikiria kuwa unaweza kufanya vyema katika muziki peke yako. Tunafaa kufanya kazi pamoja kama timu ama tutaendelea kutumika vibaya katika tamasha.”

Aliongeza kuwa umoja wa wasanii wa kutoka nje ya nchi ndiyo sababu kuu ya muziki wao kufanya vyema, si tu katika mataifa yao bali pia katika taifa letu.

“Tuangalie vile hawa wasanii wanafanya, wanaungana pamoja na kupitia umoja wao, wanaweza kuteka anga za humu nchini na mataifa yao wenyewe.”

Miaka ya awali mchekeshaji Eric Omondi amekuwa na kauli kama hii, akiwataka wanamuziki wa Kenya kutia bidii na kuacha kutumika vibaya na mapromota wa matamasha humu nchini.

View Comments