In Summary

• Ringtone alisema haikuwa sawa kwake kufurushwa nyumbani kwake ilhali ama haki kama Wakenya wengine.

• Ringtone aliwaomba msaada mashabiki wake na kuwataka kumuombea aweze kuyapiku masaibu yanayomkumba kortini.

Aliyekuwa msanii wa injili Ringtone Apoko
Image: Ringtone (Instagram)

Mwanamuziki wa nyimbo za Injili, Alex Apoko almaarufu Ringtone aliyeachiliwa siku ya Jumanne kwa dhamana alidondokwa na machozi akisimulia jinsi alivyofurushwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake.

Mwanamuziki huyo anayekabiliana na mashtaka ya shambulio mahakamani, alisema haikuwa sawa kwa yeye kufurushwa nyumbani kwake ilhali alikuwa na haki kama Wakenya wengine.

Ringtone alifichua kuwa amekuwa akiishi kwa nyumba hiyo ya kukodisha kwa zaidi ya miaka 10 sasa na alihisi kuna utaratibu uliostahili kufuatwa ili kumuondoa.

“Niko Kenya kwetu, Nimefanyiwa madhambi, sikutaka kuongea kwa sababu watu wanafikiria nadanganya. Hii ni nyumba nimekuwa nikiishi, nguo zangu, kitanda changu na kila kitu yangu iko kwa hio nyumba. Ata ukiangalia kwa video nimepost Instagram siku zote nimefanya kwa hii nyumba.”

Kulingana na Ringtone, kesi iliyo mahakamani  kwa tuhuma za kuwashambulia raia kadhaa wa Sudan na kuharibu viti vya thamani ya Sh50000 ilikuwa ya kusingiziwa na akasema alihisi kesi hiyo haikuwa sawa kwani mali anayodaiwa kuharibu ni yake.

Ringtone aliwaomba usaidizi mashabiki wake na kuwataka kumuombea aweze kuyapiku masaibu yanayomkumba kortini.

Siku ya Jumanne, Alex alifikishwa mahakani baada ya kukamatawa na polisi katika eneo la Lang’ata  na kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kuwashambulia raia kadhaa wa Sudan na kuharibu viti vya thamani ya Sh50000.

Mwanamuziki huyo alishtakiwa pamoja na Samson Onunga almaarufu Kazola, Victor B Maringa, Kevin Nyaoke, Brian Jumba Luseno na Geoffrey Mose.

Watano hao walikanusha mashtaka na kupitia kwa wakili wao waliomba wapewe masharti ya dhamana.

Hata Hivyo, mwanamuziki huyo aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000 kila mmoja.

View Comments