In Summary

• Harmonize alisema ndio maana aliamua kuachia ngoma tatu kwa mpigo ili kusambaratisha njama ya Diamond na Alikiba.

• Lakini alisisitiza kwamba anawakubali sana wawili hao na kuwataka wasirudie kufanya kile walijaribu kufanya wakilenga kumpoteza.

Diamond, alikiba na Harmonize,
Image: Instagram

Wiki hii ilianza kwa kishindo cha aina yake wasanii wanaotajwa kuwa namba moja kwenye tasnia ya Bongo Fleva Diamond na Alikiba wakipandisha joto kwa kushambuliana mitandaoni.

Sasa msanii Harmonize ametia neno kwa ugomvi huo akisema kuwa kinyume na wengi walivyouona kuwa ni wa kibinafsi, wawili hao walikuwa na njama ya kuungana ili kummaliza kimuziki.

Harmonize amefichua haya katika ujumbe mrefu aliouandika kwenye Instagram Story yake akisema kwamba baada ya kuona wakiungana ili kumpoteza katika ramani ya muziki, alilazimika kuruka ndani ghafla ili kutibua njama yao.

Harmonize alisema kuwa alilazimika kuachia ngoma tatu kwa mpigo kama njia moja ya kusambaratisha njama yao ya kujificha katika ugomvi ili kulifuta jina lake na wao kubaki wakiongelewa.

“Kiufupi hii siku nilichafuka roho sana. Kuna kaka wawili nawaheshimu sana, ila nikaanza kuona mkakati wa ghafla, muungano Fulani hivi Kigoma Allstars [kwa maana ya Diamond na Alikiba ambao wote wanatajwa kutokea Kigoma], nikasema hawa watanizoea, ngoja niwagombeze,” Harmonize aliandika.

Ila alisisitiza kwamba hana baya na Diamond wala Alikiba akisema kwamba anawaheshimu na kuwakubali sana katika kile wanachokifanya kuchangamsha genge.

“Samahani kaka zangu, msirudie, mnajua ninavyowakubali. Tuheshimiane tu,” Harmonize aliwaambia.

Mapema wiki hii tulikuripotia jinsi ugomvi wa Alikiba na Diamond ulivyoteka vichwa vya habari za udaku baada ya Diamond kwenda Instagram na kuachia ujumbe mrefu akimkashifu Alikiba kwa kuendeleza kumshambulia licha ya kuwa hamfikii kimapato.

Diamond alimdhalilisha Alikiba kwa kumuita malkia badala ya mfalme kama anavyoitwa na pia kusema kwamba kauli ya Alikiba kujiita mwenye sauti nzuri ya kuimba yaani Vocalist ni ya kujishobokesha tu kwani yeye ni mbana pua tu.

Harmonize naye amerejea na lake jipya, akizomeana vikali na aliyekuwa mpenzi wake Kajala Masanja na bintiye Paula, baada ya kuachia eimbo mpya Dear Ex.

Katika wimbo huo, Harmonize anaweka paruwanja jinsi Kajala na bintiye walimhangaisha kifedha na kumuacha hoi wakidhani ndio wamemmaliza.

 

View Comments