In Summary

• Msanii huyo alisema kwamba baadae pia Diamond na Jux pia walimshtaki kwa kampuni inayowasambazia muziki.

Diamond na Jux
Image: Instagram

Msanii Diamond Platnumz anazidi kuandamwa na pigo baada ya jingine, la hivi karibuni likiwa ni wimbo alioshirikishwa na Juma Jux, Enjoy kufutwa kwenye mtandao wa YouTube kutokana na masuala yanayofungamana na hakimiliki.

Hata hivyo, sio video ya wimbo huo iliyofutwa bali ni audio ambayo ilitoka kama wiki mbili zilizopita.

Ukienda kwenye mtandao wa YouTube, audio ya wimbo huo haipatikani na inasema kwamba wimbo huo uliondolewa baada ya mtu anayedai kuwa mmiliki halisi wa wimbo wenyewe kutoa malalamishi yake kwa YouTube.

Jamaa huyo kwa jina Sapologuano Odenumz anayedaiwa kutoka kwenye Jamhuri la Kidemokrasia ya Kongo alisema kwamba kuna vitu ambavyo Diamond na Jux waliiba kutoka kwenye wimbo wake.

Akizungumza na blogu moja maarufu sana nchini Tanzania, Odenumz alisema kwamba ni kweli alitoa malalamishi kwa YouTube kwa sababu melody za wimbo wake zilipatikana kwenye wimbo huo wa Enjoy.

“Ndio niliupiga huu wimbo chini kwa copyright kwa sababu ya melody ya wimbo wangu wa I Found Love na ilipatikana kwenye wimbo wao huo wa Enjoy,” alisema.

Msanii huyo alisema kwamba baadae pia Diamond na Jux pia walimshtaki kwa kampuni inayowasambazia muziki wao na mapambano bado yanaendelea.

Msanii huyo alisema kwamba alishtuka sana baada ya kusikiliza wimbo wa Enjoy na akaamua kumuandikia Jux kumjulisha lakini hakumjibu akisema kwamba anachokisubiri ni wao kumfuata ili waweze kuyanyoosha.

“Nasubiri wao wanicheki ili tuweze kuyamaliza kwa sababu wao pia wametumia nguvu yao na kunishtaki. Mimi nipo Kongo,”

“Wimbo huo nilitoa lalamiko kwa YouTube kitambo sana wakati wimbo umetoka lakini jana ndio wameniambia kwamba wamehsafanikisha kuufungia. Kwenye barua pepe nimeona ujumbe wakinitaka tukutane tuyamalize, mimi ninachotaka ni kulipwa tu maana ni kazi tunapambana na bado wadogo. Ni maongezi tu baada ya kuongea, siwezi kusema nataka kiasi kipi,” alisema.

View Comments